Washukiwa mauaji ya Shakahola waendelea kusota rumande
24 Julai 2023Mhubiri Paul Mackenzie na washukiwa wengine 64 wamefikishwa katika mahakama ya shanzu mjini Mombasa nchini Kenya mapema leo kusikiliza hatua ya mapendekezo ya kesi yao.
Mawakili wanaosimamia kesi hiyo walipeleka mapendekezo kuitaka mahakama kuwatangaza washukiwa hao kama waathiriwa.
Lengo la pendekezo hilo ni kutaka wasimamiwe na bodi ya ulinzi ya waathiriwa,lakini mahakama imetupilia mbali pendekezo hilo kwa hoja kuwa, wataendelea kupata ulinzi licha ya kuwa kizuizini.
Soma pia:Manusura wa Shakahola wafutiwe mashitaka- KNHCR
Mahakama hiyo imeamrisha washukiwa wote 65 waendelee kuwekwa rumande katika jela za wanawake na wanaume za Shimo la Tewa Mombasa, hadi pale uchunguzi utakapokamilika.
Mahakama pia imeamuru madaktari wanaowashughulikia mahabusu hao kuendelea kuwafanyia uchunguzi wa kimatibabu na kuwapa ushauri nasaha kila kadri wanapoona inahitajika.
Shughuli ya kutafuta miili yasitishwa
Shughuli ya ufukuaji wa miili ya wafu Shakahola imesimamishwa kwa muda. Kufikia sasa idadi ya miili iliyofukuliwa imefikia 425.
Ufukuaji huo, ulikuwa umesitishwa ili kupisha uchunguzi wa miili 87 iliyofukuliwa katika awamu ya nne.
“Kati ya maiti 16 tulizozifukua juzi Jumanne, baadhi zilikuwa bado mbichi, nguo zilizotumika kuzifunika, zilikuwa bado nzima na nyingi ni watu wazima,” Moja ya chanzo kilisema ambacho hakutaka jina lake litaje.
Miili hiyo inasemekana kuzikwakatika eneo la Kwa Mugambi. Ndiyo idadi kubwa zaidi ya miili ambayo maafisa wa upelelezi wa mauaji wamefukua katika awamu ya nne ya operesheni hiyo.
Soma pia:Maiti nyingine 11 zafukuliwa katika msitu wa Shakahola
Mtandao wa Nation umeripoti kuwa huenda miili hiyo imezikwa mwezi mmoja uliopita, wakati timu inayohusika na zoezi hilo, ilipochukua mapumziko ya wiki mbili kabla ya kuanza tena awamu nyingine ya ufukuaji zaidi ya juma moja lililopita.
Idara ya Upelelezi ya Makosa ya Jinai nchini Kenya imeanza msako kuwatafuta washukiwa kuizika miili mipya katika msitu wa Shakahola.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Rhoda Onyancha, amekanusha madai hayo akitaja kuwa hakuna miili yoyote iliyozikwa hivi karibuni.
Shughuli ya ufukuaji wa miili ya wafu Shakahola imesimamishwa kwa muda. Kufikia sasa idadi ya miili iliyofukuliwa imefikia 425.