1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la wanamgambo la kiislamu lawauwa wanajeshi 31 Niger.

10 Januari 2020

Washukiwa wa kundi la wanamgambo la kiislamu wameshambulia kambi moja ya kijeshi katika eneo la Magharibi mwa Niger jana usiku na kuwauwa takriban wanajeshi 31.

Symbolbilder Niger Armee
Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Shambulizi hilo lililenga kituo cha kijeshi katika mji wa Chinagodrar katika taifa hilo la Afrika Magharibi katika mpaka na Mali.

Awali wizara ya ulinzi ilizungumzia kuuawa kwa watu 25 hapo jana lakini baadaye ikageuza takwimu hizo kufikia watu 31 leo asubuhi.

Kulingana na taarifa iliyosomwa na msemaji wa wizara ya ulinzi ya Niger Souleymane Gazobi imesema,'' Siku ya Alhamisi tarehe 9 Januari mwendo wa saa saba mchana, kituo cha kijeshi cha Chinagodrar, katika mpaka na Mali, kilizuia shambulizi lililoongozwa na magaidi waliokuja na magari kadhaa na pikipiki. Hatua hiyo kwa usaidizi wa angani kutoka  jeshi la angani  la Niger pamoja na washirika wetu, ilituwezesha kuwashambulia adui zetu nje ya mipaka yetu. Wizara ya ulinzi, rais wa Jamhuri hii na mkuu wa majeshi, wanatuma risala zao kwa familia za waathiriwa na kuwatakia majeruhi afueni ya haraka''.

Haikubainika mara moja aliyehusika katika shambulizi hilo umbali wa kilomita 209 Kaskazini mwa mji mkuu wa Niamey.

Lakini tukio hili linasadifiana na kampeini ya makundi ya kiislamu yanayoshirikiana na al-Qaeda na kundi linalojiita dola la Kiislamu kulilazimisha jeshi la Nigeria kuondoka katika mpaka wa Magharibi na Mali ambapo udhibiti wa serikali wa eneo la Kati la Mashambani na Kaskazini umesambaratika kwasababu ya kuongezeka kwa makundi ya kijihadi.

Licha ya juhudi za vikosi vya kimataifa za kuzuia makundi hayo, mashambulizi yameongezeka mara nne zaidi katika muda wa mwaka mmoja nchini Niger na kusababisha vifo vya takriban watu 400 kulingana na takwimu kutoka kwa shirika moja lisilokuwa la kiserikali la Armed Conflict Location and Event Data Project.

Hii inajumuisha shambulizi la mwezi uliopita lililosababisha mauaji ya wanajeshi 71 katika kituo kingine cha kijeshi takriban kilomita 150 Magharibi mwa Chinagodrar, linaloaminika kuwa shambulizi baya zaidi dhidi ya jeshi la Nigeria.

Usalama umesambaratika mwaka huu katika eneo la Sahel kutokana na mashambulizi ya kijihadi na mashambulizi ya kikabila kati ya jamii pinzani za wakulima na wafugaji. Eneo hilo limekuwa katika mzozo tangu mwaka 2012 wakati waasi wa Tuareg walipoteka thuluthi mbili za eneo la Kaskazini mwa Mali na kuilazimisha Ufaransa kuingilia kati mwaka uliofuatia. Makundi ya kijihadi yamejipanga upya na kupanua ukubwa wa ushawishi wao.

 

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW