Washukiwa wa 'mapinduzi' Ujerumani wafikishwa mahakamani
29 Aprili 2024Wanachama tisa wa kundi hilo linaloongozwa na mfanyabiashara na mwanamfalme, Heinrich XIII Reuss, waliwasili kwenye mahakama ya mji wa kusini magharibi mwa Ujerumani, Stuttgart, wakisindikizwa na maafisa wa usalama siku ya Jumatatu (Aprili 29).
Miongoni mwa washitakiwa hao alikuwamo mwanajeshi mmoja wa kikosi maalum, mbunge mmoja wa zamani wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, mtaalamu mmoja wa anga za juu na mpishi mmoja mashuhuri wa hapa Ujerumani.
Katika kesi hiyo, waendesha mashitaka walikuwa wanawashutumu kwa kupanga kuipinduwa serikali ya Ujerumani.
Soma zaidi: Polisi ya Ujerumani yawasaka wanachama wa Reichbürger
Maafisa wa usalama walisema wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia wamekuwa wakiongezeka kwa kasi na wamekuwa kitisho kikubwa katika taifa hili lenye historia ya siasa za unazi.
Kutokana na uzito wa kesi yenyewe na haja ya hatua za ziada za usalama, ilibidi kesi hiyo kugawanywa kwenye mahakama tatu tafauti.
Athari za nadharia za upotoshaji
Reuss, ambaye kama mapinduzi yangelifanikiwa ndiye aliyepangwa kuwa mkuu wa nchi, atafikishwa mahakamani mjini Frankfurt mwezi Mei, ambapo watafikishwa mjini Munich mwezi Juni.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, watuhumiwa hao walikuwa wameathiriwa na mchanganyiko wa nadharia za upotoshaji zinazotokana na vuguvugu la kimataifa la QAnon na kile kiitwacho Reichsbuerger.
Vuguvugu la Reichsbuerger linawakutanisha pamoja wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia na wale wanaopigania haki ya kumiliki silaha na ambao wanakataa uhalali wa jamhuri ya sasa ya shirikisho la Ujerumani.
Wafuasi hao kwa ujumla wanaamini kwenye kuendelea kuwapo kwa kile kiitwacho Reich, ama himaya ya Ujerumani ya kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia, chini ya ufalme, na makundi kadhaa yametangaza mataifa yao wenyewe.
"Chuki dhidi ya demokrasia"
Waziri wa Mambo ya Ndani, Nancy Faeser, alisema makundi kama haya ya Reichsbuerger yanaongozwa na kile alichokiita "chuki dhidi ya demokrasia."
"Tutaendelea kuchukuwa hatua madhubuti hadi tufanikiwe kuiumbua hadharani na kuivunja mifumo yote ya Reichsbuerger." Alisema waziri huyo.
Soma zaidi: Washukiwa 25 wa siasa za mrengo wa kulia wakamatwa Ujerumani
Watuhumiwa waliopandishwa leo kwenye mahakama ya Stuttgart wanashukiwa kuwa ndio tawi la kijeshi la njama hiyo ya mapinduzi, ambalo lilipewa jukumu la kuanzisha vikosi vya ulinzi wa mipaka ya nchi.
Miongoni mwao alikuwa ni Andreas M., mwanajeshi wa kikosi maalum aliyesemekana kuwa alitumia fursa ya kuwa kwake mwanajeshi kushawishi wengine jeshini.
Kwa mujibu wa wachunguzi, kundi la Reuss linakubaliana na imani kwamba Ujerumani inatawaliwa na wanachama wa kile kiitwacho "dola la siri" na kwamba inaweza kukombolewa kwa msaada wa mtandao wa siri wa kimataifa, unaofahamika kama "muungano wa washirika."
Vyanzo: dpa, AFP