Washukiwa wa mauaji ya San Bernardino watambuliwa
3 Desemba 2015Polisi imewatambua washukiwa hao wawili kuwa ni Syed Farook, raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 28 ambaye alifanya kazi katika serikali za mitaa, na Tashfeen Malik mwenye umri wa miaka 27, ambaye uraia wake bado haujulikani. Polisi imesema washukiwa hao walikuwa wameoana au walikuwa wanachumbiana.
Mkuu wa polisi wa mji wa San Bernardino, Jarrod Burguan amethibitisha kuwa washukiwa wote wawili wameuawa, na kuwa polisi haiamini tena kuwa mshukiwa wa tatu aliyetajwa hapo awali angali mafichoni.
Washukiwa hao wawili walivamia tamasha la kufunga mwaka katika kituo kimoja cha huduma za jamii mjini San Bernardino, na kuwauwa watu 14. Wengine 17 walijeruhiwa katika tukio hilo la ufyatuaji risasi. Mkuu wa polisi Burguan amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, lakini kwa sasa ni mapema kusema kama lilikuwa tukio la kigaidi.
Kwa mujibu wa polisi, Farook alikuwa afisa wa ukaguzi wa mazingira aliyefanya kazi katika idara ya afya ya eneo hilo kwa miaka mitano. Farouk alihudhuria tamasha hilo la Krismasi lililoandaliwa na idara ya afya na akaondoka baada ya kutokea mzozo. Alirejea muda mfupi baadaye akiandamana na Malik, wakiwa na silaha nzito. "Nadhani kwa kuzingatia tulichokiona, na namna walivyokuwa wamejihami, lazima kulikuwa na kiwango Fulani cha maandalizi ambayo yalifanywa. kwa hivyo sidhani kama walikimbia nyumbani maramoja, wakavaa sare hizi za kijeshi, wakanyakua bunduki na kurejea katika tamasha kabla ya kuanza kufyatua risasi kiholela".
Mauaji hayo yamemfanya Rais Barack Obama kuzungumza kwa ghadhabu , akilitaka kwa mara nyingine Bunge la Marekani kupitisha sheria kali za kudhibiti matumizi ya bunduki ili kuzuia maafa yanayotokea kila mara nchini Marekani ya mashambulizi ya bunduki. "Kitu kimoja tunachokifahamu ni kuwa tuna muundo sasa wa mauaji ya watu wengi humu nchini ambayo hayawezi kulinganishwa na mahali kwingine ulimwenguni. na zipi hatua kadhaa tunazoweza kuchukua, sio kuyaangamiza matukio haya ya mauaji ya watu wengi, lakini kuimarisha nafasi za kuyazuia yasitokee mara kwa mara kupitia sheria za usalama wa umiliki wa bunduki"
Baraza la Uhusiano wa masuala ya Kiislamu nchini Marekani tawi la California limelaani mauaji hayo. Mauaji hayo ndiyo mabaya zaidi tangu Desemba 14 2012, wakati kija mmoja alipowauwa watu 26, wakiwemo watoto 20 katika shule ya Sandy Hook mjini Newton jimbo la Connecticut.
Aidha tukio hilo la jana limekuja chini ya wiki moja baada ya mtu aliyekuwa na silaha kuwauwa watu watatu katika kituo kimoja jimboni Colorado. Mwezi Oktoba, mtu aliyekuwa na silaha aliwauwa watu tisa kwenye chuo kimoja jimboni Oregon kabla ya kujiuwa.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri:Yusuf Saumu