1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washukiwa wa ugaidi kufikishwa mahakamani

5 Aprili 2012

Wizara ya ulinzi ya Marekani imepitisha uamuzi wa kuwafikisha mahakamani watu watano wanaoshukiwa kuwa ndio waliopanga mashambulizi ya kigaidi yaliofanyika Marekani Septemba 11, mwaka 2001.

Khalid Sheikh Mohammed
Khalid Sheikh MohammedPicha: AP

Miongoni mwa washukiwa hao ni Khalid Sheikh Mohammed, ambaye inasemekana ndiye aliyeoungoza mpango wa mashambulizi hayo ya kigaidi. Uamuzi huo wa kuwafikisha washukiwa wa mashambulizi ya kigaidi mahakamani unakuja zaidi ya miaka 10 baada ya mashambulizi yenyewe kufanyika. Wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, imeeleza kwamba inalenga kumfikisha Khalid Sheikh Mohammed na wenzake wanne katika mahakama ya kijeshi iliyoko katika gereza la Guantanamo Bay. Mahakama hiyo itadai hukumu ya kifo kwa ajili ya washukiwa hao.

Sheikh Mohammed na wenzake wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa kundi la kigaidi la al-Qaeda, watatakiwa kufika mahakamani mnamo siku 30 kwa ajili ya kusomewa mashtaka yao. Hata hivyo, inakadiriwa kwamba itachukua muda wa miezi kadhaa hadi kesi ianze kusikilizwa. Msemaji wa ikulu ya Marekani, Jay Carney, amesema kwamba ni jambo la muhimu sasa kuona hatimaye haki inatendeka.

Mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, mwaka 2001Picha: AP

Mahakama za kijeshi zapingwa

Pentagon imeeleza kwamba kesi hii sasa iko mikononi mwa mahakama ya kijeshi. Upo uwezekano wa washitakiwa wote kuhukumiwa adhabu ya kifo. Mbali na Khalid Sheikh Mohammed anayetokea Kuwait, washitakiwa wengine ni Ramzi Binalshib na Walid bin Attash kutoka Yemen, Mustafa Ahmad Al-Hawsaw kutoka Saudi Arabia na Ali abd Al-Aziz Ali anayetokea Pakistan. Washukiwa wote watano walikamatwa kati ya mwaka 2002 na 2003 na inadhaniwa kwamba walifungwa kwa miaka kadhaa katika magereza ya siri ya shirika la ujasusi la Marekani, CIA, kabla ya kuhamishiwa katika gereza la Guantanamo Bay. Mwaka 2008, chini ya utawala wa rais George W. Bush, palifanyika jaribio la kuwafikisha mahakamani.

Mashirika ya haki za binadamu daima yamekuwa yakilaumu uamuzi wa kuendesha kesi katika mahakama za kijeshi. Kwa mara nyingine tena, mashirika hayo yanadai washukiwa wa ugaidi washitakiwe katika mahama za kiraia. Naye wakili wa mshukiwa Ali abd Al-Aziz Ali, Bw. James Connel, ameeleza kwamba pasingekuwepo na uwezekano wa Ali kuhukumiwa adhabu ya kifo kama kesi yake ingesikilizwa katika mahakama ya kiraia.

Mfungwa katika gereza la Guantanamo BayPicha: dapd

Mahakama za kijeshi zilianzishwa baada ya mashambulizi ya kigaidi ya septemba 11, chini ya utawala wa George Bush, kwa sababu maafisa wa serikali walidai kwamba wanajeshi wa al-Qaeda ni kundi ambalo haliwezi kuhukumiwa katika mahakama ya kiraia. Lakini chini ya utawala wa Rais Barack Obama, utaratibu unaofuatwa katika mahakama za kijeshi umebadilishwa kwa kiasi fulani ili ufanane zaidi na utaratibu ulioko katika mahakama za kiraia.

Mwandishi: Elizabeth Shoo

Mhariri: Saumu Yusuf