1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasichana 700 waokolewa dhidi ya ukeketaji Tanzania

Hawa Bihoga5 Februari 2021

Zaidi ya watoto wa kike 700 wameokolewa dhidi ya kukeketwa katika mwaka wa 2020 na kituo cha sheria na haki za binadamu nchini Tanzania.

Symbolbild Genitalverstümmelung | Uganda
Picha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Wadau wa kampeni ya kupinga ukeketaji wamesema kuwa bado jitihada za pamoja zinahitajika ikiwemo utashi wa kisiasa katika kufikia malengo ya dunia ya kutokomeza utamaduni huo ifikapo 2030.

Wakati hayo yakijiri takwimu rasmi za serikali zinaonesha, kiwango cha ukeketaji kimepungua kutoka asilimia 18 hadi asilimia 10.1 mwaka 2015 kwa upande wa Tanzania bara huku Zanzibar ni asilimia 0.1, hatua inayotajwa na wadau wa masuala ya ukeketaji kuwa utashi wa kisiasa unanafasi kubwa katika kufikia asilimia sifuri ya ukeketaji ifikapo 2030.

Soma pia:

Ukeketaji ni nini na unafanyika wapi

Ukeketaji wa wanawake: Waathiriwa elfu 68 Ujerumani

Upasuaji kurekebisha sehemu za siri za waliokeketwa

Akizungumza na waandishi wa habari Getrude Abene afisa wanawake na watoto kutoka kituo cha sheria na haki za binadamu, anasema zaidi ya wasichana 700 mkoani Mara wameepushwa kufanyiwa ukeketaji, huku idadi kubwa kati yao wakiwa wametoroka au kutoa taarifa kabla ya kitendo hicho kufanikiwa, hatua walioitaja kuwa elimu ya kupinga mila hiyo  dhalimu imetamalaki kwa umma.

Abene ameongeza kuwa chagamoto inayowakabili kwa hivi sasa ni pamoja na uhaba wa nafasi katika nyumba salama ambazo watoto wanahifadhiwa kabla ya kurejeshwa katika familia zao huku wakiendelea kushirikiana na jeshi la polisi kuangalia usalama wa wasichana hao.

Jamaa akiwa amevaa tisheti iliyoandikwa komesha ukeketajiPicha: Reuters/S. Modola

Ili kufikia lengo la kutokomeza vitendo vya ukeketaji ulimwenguni, umoja wa mataifa unataja kuwa, itahitajika dola bilioni 2.4 hii ni katika kipindi cha mika 10 ijayo ambapo kila msichana mmoja atatumia kiasi cha dola mia moja ikitajwa ni fedha kidogo katika kulipa ili kuokoa thamani ya msichana.

Katika wito wa pamoja uliotolewa na shirika la idadi ya watu ulimwenguni UNFPA na shirika la kuhudumia watoto la umoja wa mataifa UNCEF wamesema lazima kila mmoja achukue hatua ya kusema imetosha na kuwalinda wasichana dhidi ya mashambulio ya ukeketaji katika miili yao. Wito huo umesisitizwa na Warren Bright ambaye ni mkuu wa mawasiliano UNFPA alipozungumza na waandishi wa habari.

Kila ifikapo Februari 6 dunia huadhimisha siku ya kutokomeza mila ya ukeketaji, kauli mbiu ya mwaka huu ni 'Hakuna muda wa kupoteza' kuchukua hatua kutokomeza kadhia hiyo.

Vita dhidi ya utamaduni wa kuwakeketa wasichana katika jamii ya Wamaasai

02:33

This browser does not support the video element.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW