Wabakwa na kuchoma moto Sudan Kusini
30 Juni 2015Wachunguzi wa haki za binaadamu kutoka Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini - UNMISS, wameonya kuhusu kufanyika "matukio mengi ya ukiukaji wa haki za binaadamu" katika ripoti yao iliyowashirikisha waathiriwa 115, na mashuhuda kutoka jimbo la kaskazini la Unity, ambalo limeshuhudia mashambulizi makali katika siku za karibuni tangu kuanza vita vya wenyewe kwa wenyewe miezi 18 iliyopita.
Jeshi la Sudan Kusini - SPLA lilianzisha operesheni kubwa dhidi ya wanajeshi waasi mnamo mwezi Aprili, huku kukiwa na mapigano mikali katika wilaya ya Mayom, kaskazini mwa jimbo la Unity, ambalo wakati mmoja lilikuwa eneo muhimu kwa uzalishaji wa mafuta.
Walionusurika katika mashambulizi hayo walisema kuwa majeshi ya SPLA na magenge ya wapiganaji yaliwaua raia, kupora katika vijijini na kuwaacha zaidi ya watu 100,000 wakiwa hawana makazi.
Wachunguzi walisema walikusanya angalau matukio tisa tofauti ambapo wanawake na wasichana walioteketezwa kwa moto katika vibanda baada ya kubakwa na makundi ya wabakaji ikiwa ni ishara ya visa vya unyanyasaji wa kijinsia, na kujumuisha matukio kadhaa ya akina mama kubakwa mbele ya watoto wao na wengine walipigwa risasi na kuuliwa baada ya kubakwa.
Ripoti ilieleza, Shahidi mmoja alieleza alivyoona makundi ya vikosi vya serikali yakimbaka mama aaliyekuwa akimnyonyesha mwanawe, baada ya kumtupa mtoto wake kando, na shahidi mwingine alielezea jinsi askari walivyowalazimisha wanawake kulibinya makaa ya moto kwenye viganja vya mikono yao.
Vikosi vya waasi pia wamekuwa watuhumiwa wa kufanya mauaji, ubakaji na kuajira wanajeshi watoto.
Hakukuwa na jibu la haraka kutoka kwa jeshi, ambapo awali lilikanusha madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu.Umoja wa Mataifa ilisema ripoti ilikabidhiwa kwa viongozi wa serikali, ambao bado hawajatoa maoni juu ya matokeo ya utafiti huo.
Umoja wa Mataifa ilisema walijaribu kutembelea maeneo yalikofanyika mauaji ambayo yalielezwa na mashahidi, lakini mara nyingi walikataliwa kuingia na jeshi, lakini kulikuwa na uthibitisho wa taarifa kutoka vyanzo kadhaa.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini vilizuka mwezi Disemba mwaka 2013 baada ya rais Salva Kiir kumshtumu makamu wake wa zamani Riek Machar kwamba aliandaa mpango wa kumpinduwa.
Miaka minne sasa tangu Sudan Kusini kupata uhuru wake, theluthi mbili ya idadi ya watu milioni 12 wanahitaji msaada,ikiwa ni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, na kila mkazi mmoja kati ya sita ameyakimbia makazi yake.
Mwishoni mwa juma lililopita Rais Salva Kiir alikutana na Riek Machar na kufanya mazungumzo Nairobi nchini Kenya na kujadili namna ya kurejesha amani na uthabiti wa taifa, lakini msemaji wa waasi Mabior Garang anasema mazungumzo hayo hayakuwa na matokeo yoyote.
Mwandishi:Salma Mkalibala/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman