Wasichana zaidi wa shule Iran walishwa sumu
6 Machi 2023Kumekuwa na msururu wa visa kama hivyo nchini humo, jambo lililozusha hofu miongoni mwa wazazi wanaoitaka serikali kuchukua hatua sasa.
Visa hivyo vya ulishwaji sumu vilivyowapelekea baadhi ya wasichana kulazwa hospitali, vimekuwa gumzo la kitaifa nchini humo huku naibu waziri wa afya Younes Panahi akisema wiki iliyopita kwamba visa hivyo vinalenga kuzifunga shule za wasichana ili wasipate elimu.
Katika ripoti moja iliyorushwa na shirika la habari la kitaifa nchini Iran, mama wa msichana mmoja ambaye ni mhanga wa matukio hayo, amezitaka mamlaka nchini humo kuweka mlinzi katika lango kuu la kila shule na kutaka kamera za siri zilizo katika shule kuanza kufanya kazi.
Shule 52 kote Iran zimeathirika na visa hivyo
Visa vya hivi karibuni vimewaathiri wanafunzi katika mji wa magharibi wa Abhar na mji wa kusini magharibi wa Ahvaz. Wasichana wa shule za msingi pia katika mji wa magharibi wa Zanjan wamelengwa na visa zaidi kuripotiwa katika mji wa Mashhad ulioko kaskazini mashariki, mji wa Isfahan ulioko eneo la kati la Shiraz kusini mwa nchi.
Tangu mwezi Novemba, sehemu kubwa ya visa hivyo vya sumu vimekuwa vikiripotiwa katika mji wa Qom, ulioko kusini mwa Mji Mkuu Tehran huku hesabu ikionyesha ni shule 52 kote nchini humo zilizolengwa na visa hivyo vya sumu.
Rais Ebrahim Raisi amesema ametoa wito kwa waziri wa usalama wa ndani kuvifuatilia visa hivyo na kufanya uchunguzi kwa kile alichokitaja kuwa "njama ya adui ya kuzusha hofu na kukata tamaa" miongoni mwa watu nchini humo.
Waziri huyo Ahmad Vahidi hapo juzi Jumamosi wakati wa kufanya utafiti wa visa hivyo, alisema kwamba wamegundua vitu fulani wanavyovitilia mashaka ingawa hakutoa taarifa zaidi kuhusiana na hilo.
Waziri wa elimu aomba msamaha
Waziri wa elimu Yousef Nouri aliomba radhi katika televisheni kwa matukio hayo akisema wanafahamu hofu ya wazazi na kwamba wanalifuatilia suala hilo.
Kwa miezi mitatu sasa, mamia ya wasichana wa shule wameripoti kupata dalili kama kushindwa kupumua na homa ya asubuhi, baada ya kuvuta harufu fulani mbaya wasizozifahamu.
Visa hivi vinafanyika zaidi ya miezi mitano baada ya kuanza kwa maandamano yaliyochochewa na kifo cha mwanamke mmoja mwenye asili ya Kikurdi aliyekuwa na umri wa miaka 22 Mahsa Amini ambaye alifariki mikononi mwa polisi kwa kudaiwa kuvaa mavazi yanayokwenda kinyume na maadili.
Chanzo: AFP