1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasifu wa Abdikadir Hussein Mohammed: Ujerumani yamtunza "Obama wa Kenya"

20 Oktoba 2011

Tuzo ya Ujerumani kwa Afrika mwaka huu wa 2011 inakwenda kwa mwanasiasa kijana wa Kenya, Abdikadir Hussein Mohammed, anayejuilikana kwa jina la utani la Obama wa Kenya. Lakini ni nani mwanasheria huyu aliyegeukia siasa?

Abdikadir Hussein Mohammed akizungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi.
Abdikadir Hussein Mohammed akizungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi.Picha: DW

Akiwa na umri wa miaka 40, tayari Abdikadir Hussein Mohamed ni mbunge wa Mandera ya Kati na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu maswala ya sheria na utekelezaji haki na mwenye hamu ya mabadiliko nchini Kenya.

Ufanisi wake katika siasa umetokana na maadili yake ya kuzingatia haki za binadamu na ari yake ya kupenda mabadiliko.

“Nchi hii ina vijana wengi wanaotamani kuongoza. Nadhani tumefikia wakati ambapo tutakuwa na mabadiliko ya uongozi kutoka kizazi kilichoakuwepo wakati nchi hii ilipopata uhuru hadi kizazi kipya kilichotokea baada ya uhuru na sioni msukumo huu uko Kenya pekee bali unaokana kote barani Afrika”. Anasema Abdikadir.

Abdikadir Mohammed ni kielelezo sio tu kwa kizazi kipya, bali kwa jamii nzima, wakubwa kwa wadogo.

Kwa Wakenya, Abdikadir ni kigezo chema

Alfred Kiti wa Deutsche Welle (kulia) akizungumza na Abdikadir Hussein Mohammed.Picha: DW

Wakenya wengi wanamuona Abdikadir kama kiongozi anayeweza kuipandisha Kenya katika upeo wa juu zaidi.

Kwa mfano, John Kuria anasema Abdikadir ameleta mabadiliko nchini Kenya "na tunaona vijana wana maono makubwa. Tukiiga mfano wa Abdikadir kilakitu kitakuwa sawa!”

Maggie Mungai anasema mwanasiasa huyu kijana amedhihirisha kwamba akili za vijana zinaweza kwenda mbali kusaidia wengine kutimiza yale wanayoyatamani. "Bila shaka ningependa kuona mengi zaidi kutokakwake kwani naamini anaweza kufanya makubwa”.

Hata Lucy Mutinda, mshauri mhandisi wa miradi ya kimazingira, ana maoni sawa na hayo. “Kusema kweli amekuwa mfano mzuri kwetu sisi vijana, katika yale tunayoyatamani ili tuweze kuchukua hatamu za uongozi”.

Kutoka Rahimu School hadi Hawarad University

Rais Barack Obama wa Marekani. Abdikadir Mohammed pia huitwa kwa jina la "Obama wa Kenya"Picha: dapd

Abdikadir Hussein alikulia katika pembe ya Kenya karibu na mpaka wa Somalia na Ethiopia. Alisoma katka shule ya msingi ya Rahimu kati ya mwaka 1977 na 1983 na baadaye akajiunga na shule ya upili ya Alliance mjini Nairobi kati ya mwaka 1984 hadi 1987. Alisomea masomo ya kidato cha tano na sita mwaka 1988 na 1989 katika shule ya Sheikh Ali. Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kusomea sheria mwaka 1990 hadi mwaka 1993.

Baada ya kuhudumu kama mwanasheria kwa muda wa miaka minne, Abdikadir alijiunga na Chuo Kikuu cha Harvard na kufuzu na shahada ya uzamili ya uanasheria.

Mara nyingi mbunge huyu wa Mandera ya Kati amelinganishwa na Rais Barrak Obama wa Marekani na kupewa jina la utani la ‘Obama wa Kenya.” Mwenyewe anasema hiyo ni kejeli..

“Profesa mmoja wa sheria kutoka New York aliandika taarifa moja kwenye gazeti akinilinganisha na mtu huyu mkubwa. Huo ni utani tu! Cha kushangaza ni kwamba tunatumia jina moja la Hussein. Alisomea chuo kikuu cha Harhard miaka kumi kabla ya mimi kuingia huko. Ni utani huo. Nisingependa kulinganishwa na kiongozi huyo, lakini langu ni kumtakia kila la kheri kwani najua yeye pia anaingia kwenye uchaguzi mwaka ujao”.

Joho la uanasheria kwenye moyo wa mwanasiasa

Abdikadir Hussein MohammedPicha: DW

Tajriba ya kisiasa ya Abbdikadir Hussein Mohamed ilianzia mwaka 2007 aliposhawishiwa na wasomi wenzake kutoka jimbo lake, awanie kiti cha bunge cha Mandera ya Kati. Alifuata ushauri huo na akambwaga kigogo wa jimbo hilo wakati huo, Billow Kerrow, wa chama cha KANU.

Mara tu baada ya wimbi la ghasia za baada ya uchaguzi kutua, mbunge huyo wa Mandera ya Kati alichaguliwa kuongoza kamati ya bunge kuhusu maswala ya sheria na utekelezaji haki nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Paul Muite wa Safina aliyepoteza kiti chake cha Kabete kwenye uchaguzi huo wa mwaka 2007.

Kutokana na bidii yake na kujitolea kwake kutekeleza majukumu aliyopewa na bunge, Abdikadir amejizolea sifa nyingi sio kwa Kenya tu, lakini hata nje ya mipaka ya nchi hiyo.

Ujerumani yautambua mchango wa Abdikadir

Rais Christian Wulff wa Ujerumani kukabidhi Tuzo ya Ujerumani kwa Afrika 2001 kwa Abdikadir Hussein Mohammed.Picha: dapd

Juhudi za kamati anayoiongoza zilizopelekea kuandikwa kwa katiba mpya zimemfanya atunukiwe tuzo ya mwaka huu ya Ujerumani kwa ajili ya Afrika, The German-Africa Prize 2011.

Abdikadir anaiona tuzo hii kama sehemu muhimu ya kutambuliwa kwa mchango wake. “Inanitia moyo mimi binafsi, kwa wanachama wa kamati yangu, wabunge, kwa nchi nzima na bara la Afrika kwa ujumla. Utambuzi huu wa serikali ya Ujerumani, watu wa Ujerumani na kamati iliyoteua mshindi wa tuzo hii, unamaanisha mambo mengi kwangu".

Kuhusu mipango yake ya baadaye ya kisiasa, Abdikadir anasema ingawaje uongozi wan chi una changamoto zake, asingejali kuongoza nchi ifikapo mwaka 2012, lakini hilo analiachia wakati umuamulie.

“Uamuzi huo nauacha wazi kwa sasa. Naweza nikatangaza chochote lakini wakati haujafika. Sina shaka kwamba lolote litakalofanyika wakati huu litaathiri hatima ya nchi hii”.

Ama agombee uraisi hapo mwakani au la, Abdikadir Hussein Mohammed anaendelea kubakia kama ishara ya umoja kwa kizazi kipya na mwakilishi wa wasomi katika tabaka la wanasiasa. Na ukweli mmoja unabakia wazi, kwamba matumaini ya mwanasiasa huyu kijana ni makubwa kuliko fikra za watu wengi.

Mwandishi: Alfred Kiti/DW- Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef