210809 Merkel-Porträt BTW
14 Septemba 2009
HISTORIA YAKE
Angela Merkel alizaliwa kama Angela Dorotea Kasner mnamo Julai 17 mwaka 1954 mjini Hamburg katika iliyokuwa Ujerumani Magharibi. Babake aliitwa Horst Kasner na alikuwa mchungaji wa kanisa la Kiluteri. Mamake aliitwa Herlind Jentzsch na alikuwa mwalimu wa lugha ya Kiingereza na Kilatin.
Mnamo mwaka 1977 Angela Dorotea Kasner aliolewa na mwanafunzi wa Fizikia, Ulrich Merkel, na hivyo kubadilisha jina lake na kuitwa Angela Dorotea Merkel. Ndoa hiyo ilimazikia kwa talaka mnamo mwaka 1982. Mume wake wa pili, Joachim Sauer, ni mwanakemia na profesa.
Novemba 22 2005 Angela Merkel alikula kiapo kuwa kansela mpya wa Ujerumani, na hivyo kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo. Muongo mmoja na nusu kabla, katika iliyokuwa Ujerumani ya Mashariki, DDR, kansela Merkel alijisajili katika kundi la upinzani la kanisa la kiinjili kama mtaalam wa sayansi ya kimaumbile. Waziri mkuu wa kwanza wa Ujerumani Mashariki kuchaguliwa katika uchaguzi huru, Lothar de Maiziere, alimteua Angela Merkel kuwa makamu msemaji wa serikali. Baada ya uchaguzi wa ukansela mwishoni mwa mwaka 1990, Merkel alipendekezwa kwa kansela Helmut Kohl,ambaye alimteua Angela Merkel kuwa waziri wa wanawake na vijana. Angela Merkel alifanya kazi katika ngazi ya juu ya chama chake na baadaye mwaka 2005 akachaguliwa kuwa kansela ambapo Merkel mwenyewe alisema
"Kwamba mtu kama mimi, mwanamke kutoka iliyokuwa Ujerumani Mashariki, naweza kuwa kansela wa Ujerumani, hilo kwangu baada ya miezi 10 tangu kuingia madarakani, limekuwa jambo la kawaida. Kwa upande mwingine katika siku kama hii ya leo, ni jambo lengine la kipekee."
Ukweli ni kuwa katika uchaguzi wa mwaka 2005 nia ya kuwa na serikali ya muungano wa vyama vya CDU na CSU pamoja na chama cha kiliberali cha FDP, haikutimia. Lakini hata hivyo chama cha Social Democratic, SPD, kilichounda serikali pamoja na muungano wa vyama vya CSU na CSU, kilishirikiana vizuri na kansela Merkel. Ili kuweza kupunguza deni kubwa lililoikabili nchi, serikali ya mseto iliongeza kodi ya mauzo kwa asilimia tatu, uamuzi ambao kwa chama cha SPD ulikuwa mgumu kuukubali.
MCHANGO WAKE KATIKA KATIBA
Mchango wa kansela Merkel kuhusu katiba mpya ya Ulaya ni mojawapo ya ufanisi wa sera za nje za Angela Merkel, ambazo zimemfanya kuwa mwanasiasa wa Ujerumani anayependwa zaidi. Hata ufanisi wake ndani ya nchi umemfanya Angela Merkel kuwa maarufu: Ukosefu wa ajira umekuwa ukipungua tangu Merkel alipoingia madarakani kwa takriban nafasi milioni mbili, na mnamo mwaka 2007, kwa mara ya kwanza katika miongo kadhaa, Ujerumani ikaongeza fedha kwa ajili ya bima ya kijamii. Baadaye mgogoro wa kiuchumi ukapiga hodi Ujerumani. Kansela Merkel na serikali yake alianzisha mpango maalum wa kuyaokoa mabenki yasifilisike uliogharimu mabilioni ya euro mpango huo ukaanzishwa katika awamu ya kwanza na ya pili.
MUONEKANO WAKE KWA WAHAFIDHINA WA CDU
Waziri mkuu wa jimbo la Baden- Württemburg, Günter Oettinger, anaelezea jinsi wengi katika chama cha CDU wanavyofikiria.
"Ni kansela wa mseto mkubwa, na ndio maana ninatarajia kutoka kwake kwamba awe kansela anayeweza kufikia makubaliano. Lakini kama mgombea ukansela na mwenyekiti wa chama katika uchaguzi mkuu ujao, anapaswa aonyeshe wazi taswira halisi ya muungano wa CDU na CSU."
Angela Merkel anabakia mwanasiasa mahiri na aliye na msimamo imara. Jambo moja tu linalomtia wasiwasi ni ikiwa wafuasi wake na wapiga kura wa Ujerumani wanaweza kumhakikishia ushindi katika uchaguzi ujao!
Mwandishi: Josephat Charo
Mhariri: Abdul-Rahman