Wasiochanjwa Ujerumani kuzuiwa baadhi ya huduma muhimu
3 Desemba 2021Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametangaza hatua hizo baada ya kukutana na viongozi wa shirikisho na majimbo, wakati taifa kwa mara nyingine likirekodi visa vipya elfu 70,000 ndani ya saa 24. Merkel amesema hatua hizo ni muhimu katika kuelezea wasiwasi kwamba hospitali zinaweza kufurika wagonjwa wanaotaabika na maambukizi ya Covid-19, ambayo yana uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa mbaya miongoni mwa watu wasiochanjwa.
"Tunauweka mfumo wetu wa afya kwenye majaribio tena na wagonjwa wengi hawawezi kufanyiwa upasuaji kwa magonjwa ambayo hayahusiani na Covid-19. Hii inapaswa kutufanya sote kutaka kuvunja wimbi hili la nne haraka. Lakini tunalifanyia kazi na hata kama sipo tena, kazi itaendelea."COVID: Je kirusi cha omicron ni hatari kiasi gani?
Kansela huyo ameongeza kwamba bunge litajadili pendekezo la ulazima wa kuchanjwa na endapo litapitishwa basi agizo hilo litaanza kutumika mapema mwezi Februari.
Kwingineko, visa vya kwanza vya kirusi cha Omicron tayari vimeripotiwa nchini Marekani na Australia na kuongeza wasiwasi juu ya aina hiyo mpya ya kirusi cha Covid-19. Visa hivyo vinaripotiwa mnamo wakati Rais Joe Biden akitangaza mikakati mipya ya kukabiliana na Covid-19 wakati wa majira ya baridi, ikiwemo masharti ya upimaji kwa wasafiri na kuongeza kasi ya utoaji chanjo.
Uingereza nayo siku ya Alhamisi ilisema kuwa imebaini visa 10 vya Omicron na kufanya maambukizi jumla ya kirusi hicho kufikia 42.
Shirika la usalama la afya la Uingereza lilisema kumekuwa na watu wengine saba waliogunduliwa na Omicron nchini humo, na kesi tatu zaidi zimetambuliwa nchini
Scotland.
Shirika la afya la Umoja wa Ulaya limeonya kwamba kirusi cha Omicron kinaweza kusababisha zaidi ya nusu ya visa vya Covid-19 barani Ulaya ndani ya miezi michache ijayo.
Wakati huo shirika la afya ulimwenguni WHO limezionya nchi za kanda ya Asia-Pasifiki kuimarisha uwezo wa kiafya na kuwachanja kikamilifu watu wake ili kujiandaa na maambukizi ya Covid-19 wakati kirusi cha Omicron kikisambaa kote ulimwenguni.
Kirusi cha Omicron kiliingia Asia wiki hii na tayari maambukizi yameripotiwa huko India, Japan, Malaysia, Singapore na Korea Kusini.
Ingawa WHO imesema kuwa inaweza kuchukua wiki kadhaa kubaini kama Omicron inaambukiza zaidi, na kama inasababisha athari zaidi, lakini utafiti mpya wa awali wa Afrika Kusini unapendekeza kuwa kuna uwezekano mara tatu zaidi wa kusababisha tena maambukizi ikilinganishwa na aina ya Delta au Beta.
Vyanzo: ap/afp/reuters