Wasiwasi juu ya hali ya afya ya Rais Yar'adua wa Nigeria
12 Januari 2010Rais Umaru Yar'adua wa Nigeria amezungumza leo baada ya wiki saba zilizoghubikwa na kimya kingi na hofu kwa WaNigeria. Rais Ya'radua ana matatizo ya ugonjwa wa moyo na yuko nchini Saudi arabia anakopewa matibabu. .
Rais Umaru Yar'adua amekuwa hospitalini katika mji wa Jeddah tangu tarehe 23 Novemba mwaka jana. Takriban wiki saba ambazo zimechimbua maswala mengi yakiwemo uwezo wa kiafya wa rais Yar'adua kuliongoza Nigeria na pia mchakato wa kisiasa unaoleta utata kikatiba.
Hii leo mamia ya waandamanji waliobeba mabango na kukariri mistari yenye uzito wa upinzani dhidi ya rais Yar'adua, walipita katika barabara kuu za jiji la abuja. Mistari kama ' tumechoshwa… Yar'adua tuzungumzie' yalitamalaki katika vinywa vya waandamanaji hasa wanaounga mkono mrengo wa upinzani nchini Nigeria.
Kitovu cha maandamano hayo kilikuwa kumtaka rais Yar'adua ajiuzulu kwa misingi ya kiafya ili makamu wa rais, Goodluck Jonathan, aweze kuiongoza nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta na idadi ya zaidi ya raia milioni mia moja ishirini na nne katika majimbo 36.
Swala la marekebisho ya katiba limezuka huku wanasheria na mawakili wakidai kutokuweko huku kwa rais ni hatari kwa usalama wa nchi. Tayari mawakili kadhaa wanaoegemea upande kambi ya upinzani wamewasilisha kesi mahakamani kumtaka rais Yar'adua amwachie mamlaka makamu wa rais.
Mawakili hawa wanasema kwamba kifungu cha 145 cha katiba ya Nigeria, kinadokeza utaratibu wa uongozi na rais angefaa kuandika barua rasmi kumwachia makamu wake ashikilie nyadhifa ya uongozi hadi atakaporejea. Rais Yar'adua aliyezungumza kwa njia ya simu katika mahojiano na shirika la BBC alisema anapata nafuu:
"Kwa sasa naendelea kupata matibabu na kupata nafuu…. natumai hivi karibuni nitapata afueni ya haraka ili nirejee nyumbani. Wakati huu nataka kuwashukuru Wanigeria kwa maombi yao kwangu na kwa nchi ya Nigeria. Pindi tu madkatari wangu watakaponiruhusu kutoka hospitalini, nitarudi Nigeria na kutekeleza majukumu yangu ".
Kati ya matukio yaliyowapa waandamanaji hao sababu kuu ya kukereka, ni mkwamo wa kikatiba kinachompa rais uwezo wa kipekee wa kuwateua maafisa wa serikali katika ngazi ya juu. Kwa mfano, Jaji mkuu alistaafu mwishoni mwa mwaka jana, lakini inambidi aendelee kutekeleza majukumu yake hadi mwanasheria mwingine atakapoteuliwa na kuapishwa na rais.
Hali ya kiafya ya rais Umaru Yar'adua, mwenye umri wa miaka 58, imekuwa ikiathirika mno tangu ashikilie nyadhifa ya urais. Sasa ana ugonjwa wa moyo na awali alikuwa na matatizo ya figo.
Kuzungumza huku kunaondoa hofu iliyotanda kutokana na magazeti kwenye mtandao nchini nigeria yaliyokuwa na uhariri kuhusu aidha kufariki kwa rais Yar'adua au kusita kufanya kazi kwa ubongo wake.
Hata hivyo, wachunguzi wa kisiasa nchini humu wansisitizwa kuwa ingawa kuzungumza kwake kumetoa afueni kwa WaNigeria, kukosekana kwake katika kuendesha shughuli za kitaifa kunasababisha pengo hatari la uongozi.
Mshindi wa tuzo la Nobel la fasihi kwa mwaka wa 1986, na ambaye amekuwa msitari wa mbele katika mchakato wa kupigania demokrasia nchini Nigeria, Wole Soyinka, akihutubia umati wa waandamanji, alisema kutokuwepo kwa rais kunachimbua maswala mengi kitaifa. Wole Soyinka aliongezea kuwa ingawa rais ni mgonjwa, bado wanatoa changamoto kwake kuhusu visa vingi vya makampuni yaliyopewa zabuni za serikali vinavyoendelea kuzorotesha sifa ya Nigeria.
Bunge bunge la Nigeria lilirejelea vikao vyake jumanne kujadili kwa kina pengo hili la kisiasa na uongozi. Vyombo vya habari vinadai kwamba wachunguzi watatumwa nchini Saudi arabia kuangalia hali yake, kisha bunge litathmini mwelekeo utakaochukuliwa.
Msemaji wa chama kikuu cha upinzani cha Congress, Lai Mohamed, amesema kwamba ingawa wanafurahi rais anapata nafuu, chaguo lake la kutoa habari ya hali yake kupitia shirika la habari la nje linasikitisha.
Mwandishi, Peter Moss/AFP/BBC
Mhariri, Othman Miraji