1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIraq

Wasiwasi juu ya kuongezeka kwa makundi ya kigaidi Iraq

Bakari Ubena Cathrin Schaer
28 Agosti 2025

Wanasiasa wa Iraq wanapendekeza mageuzi ya sheria kuhusu wanamgambo wasio chini ya serikali, lakini wakosoaji wanaonya kuwa mageuzi hayo huenda yakaimarisha makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Iran.

Irak | Soldat der irakischen Truppen
Mwanajeshi wa Iraq akishika doria mjini KirkukPicha: Ali Makram Ghareeb/Anadolu Agencypicture alliance

Wanasiasa wa Iraq wanalenga kufanya mageuzi ya sheria inayowahusu wanamgambo walio nje ya udhibiti wa serikali. Wakosoaji wanasema mageuzi hayo ambayo yanachukuliwa kama kipimo cha uhuru wa Iraq yatazidisha uwepo wa "makundi ya kigaidi" yanayofadhiliwa na Iran nchini humo.

Marekani imetishia kuiwekewa vikwazo Iraq iwapo mageuzi hayo yatapitishwa. 

Mwishoni mwa juma, muswada wa sheria hiyo mpya na yenye utata iliwasilishwa kwa bunge la Iraq baada ya miezi kadhaa ya mivutano ya kisiasa. Sheria hiyo inalenga kufanya mageuzi kuhusu suala zima la udhibiti wa wanamgambo nchini Iraq, hasa wale wanaoitwa Popular Mobilization forces (PMF).

Ikiwa sheria hiyo itapitishwa, wakosoaji wanatabiri kuwa itakuwa na matokeo mabaya. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetahadharisha kuwa sheria hiyo itawezesha "makundi ya kigaidi" yenye silaha ambayo hudhoofisha uhuru wa Iraq kuwa sehemu ya jeshi la taifa.

Je, rasimu hiyo ya sheria inahusu nini?

Hata hivyo, wale wanaounga mkono muswada huo wana maoni tofauti. Wanasema sheria hii mpya inaweza kuwa njia ya kuyajumuisha makundi yenye silaha katika taasisi za serikali.

Renad Mansour, mkuu wa mpango kuhusu Iraq katika taasisi ya wataalam ya Uingereza, Chatham House, amesema hatua hiyo inaweza hatimaye kuiwezesha Iraq kujikomboa kutoka kwenye ushawishi wa karibu miongo miwili wa Iran kwenye siasa zake.

Muswada huo unaojadiliwa mno, kwa hakika ni marekebisho ya sheria iliyopo na inayofahamika kama sheria nambari 40 ya mwaka 2016 na inaruhusu wanamgambo wa PMF kuwa sehemu ya wanajeshi wa Iraq.

PMF ilianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2014 wakati viongozi wa kidini walipotoa wito kwa wanaume wenye uwezo kuweza kupambana na kundi la itikadi kali linalojulikana kama Dola la Kiislamu (IS).

Iraq kwatibuka tena

01:08

This browser does not support the video element.

Tangu wakati huo, vikundi vya PMF vimekuwa na nguvu na ni sehemu ya mfumo wa ulinzi wa Iraq. Lakini baadhi ya vikundi vya PMF vinaendesha shughuli zao bila kuwa chini ya udhibiti wa serikali.

Vikundi hivyo vimekuwa vikitangaza kuwa chini ya uongozi wa kidini na kijeshi wa Iran kwa sababu Tehran imekuwa ikiwapatia msaada wa kifedha, kiroho na hata vifaa. Sasa vinajinasibu kuwa sehemu ya kile kinachojulikana kama "mhimili wa upinzani wa Iran" ambao unajumuisha pia makundi ya Hezbollah huko Lebanon, Wahouthi huko Yemen na Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Baadhi ya wakosoaji, wanasiasa na hata raia wanasema muswada huu mpya unatoa kipaumbele zaidi kwa Iran kuliko Iraq, huku Marekani yenye zaidi ya wanajeshi 2,000 nchini Iraq ikipinga hatua hiyo kwa kuwa makundi ya PMF yamekuwa yakihusishwa na mashambulizi dhidi ya kambi za Marekani huko Iraq na Jordan.

Rasimu hii mpya inayofahamika kama "sheria ya PMF" - inalenga kurekebisha sheria ya awali ya mwaka 2016, ambayo ilikuwa haielezi kwa undani kuhusu jukumu la makundi hayo ya wanamgambo wa PMF jambo ambalo lilikuwa chanzo cha mizozano na kuzusha utata kuhusu masuala ya uongozi, usimamizi wa bajeti na ushirikiano katika mfumo wa usalama wa taifa, mambo ambayo yanatarajiwa kuwekwa wazi katika sheria hii mpya inayopendekezwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW