1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi juu ya Rwanda kupanua ushawishi wake Afrika

António Cascais Jacob Safari
29 Septemba 2021

Huku kampeni ya kijeshi ya kupambana na ugaidi ikiwa inaendelea kaskazini mwa Msumbiji, Rwanda inapanua ushawishi wake kisiasa, kijeshi na kijasusi katika eneo hilo. Makundi ya kiraia yanashikwa na wasiwasi mkubwa.

Mosambik | Besuch Filipe Nyusi und Paul Kagame in der Provinz Cabo Delgado
Picha: Simon Wohlfahrt/AFP/Getty Images

Rais wa Rwanda Paul Kagame  mnamo Septemba 24 alitembelea mji wa Pemba, ambao ndio mji mkuu wa eneo la Cabo del Gado. Cha kushangaza ni kwamba alikaribishwa kama mgeni maalum kwa heshima za kijeshi ila hakukuwa na nafasi ya mwenyeji wake Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi katika zulia jekundu. Anatembea kifua mbele nchini Msumbiji kwa sasa kwa kuwa nchi yake ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupeleka majeshi nchini humo kukabiliana na wanamgambo wa Kiislamu.

Lakini baadhi ya watu nchini Msumbiji wanautazama kwa wasiwasi usuhuba huu mpya kati ya nchi yao na Rwanda. Mkuu wa Kituo cha Demokrasia na Maendeleo CDD ambayo ni makundi ya kutetea haki za binadamu nchini Msumbiji, Adriano Nuvunga, ameiambia DW kuwa ni aibu kwa Msumbiji kumkaribisha kwa zulia jekundu rais ambaye amekuwa akikiuka haki za binadamu.

"Tangu vikosi vya Rwanda viingie Cabo Delgado, Kagame amekuwa akichukuliwa kama mtu wa kipekee na jambo hili linazidi. Kwa mfano tuna taarifa kwamba Msumbiji imeikubalia Rwanda kuikagua na kuilinda anga ya Msumbiji wakati wa ziara ya Kagame."

Ila Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi anausifu ushirikiano wa Msumbiji na Rwanda. Katika mkutano wa viongozi hao na waandishi wa habari aliutaja kama mfano wa kuigwa na mataifa mengine yote ya Afrika.

Vikosi vya Rwanda nchini MsumbijiPicha: Jean Bizimana/REUTERS

Takribani wanajeshi elfu moja wa Rwanda wamekuwa wakishirikiana na serikali ya Msumbiji katika mapambano yake na wanamgambo katika eneo lililo na utajiri wa mali asili la Cabo Delgado tangu mwezi Julai. Kwa siku chache tu baada ya kuingia kwao, jeshi la Rwanda liliwashambulia na kuwashinda pakubwa magaidi waliokuwa wamechukua udhibiti wa mji muhimu wa Mocimboa kwa zaidi ya mwaka mmoja. Kutokana na hilo, Kagame alipata jukwaa la kupiga propaganda. Katika serikali ya Msumbiji sasa hivi, majeshi ya Rwanda yanachukuliwa kama wafalme.

Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yanahofu kwamba kutakuwa na athari za kuhusika kwa jeshi la Rwanda katika mpango huo. Mwanaharakati Nuvunga anaamini kwamba Rwanda inatumia ushawishi wake kukandamiza wapinzani wa Rwanda nchini Msumbiji. Anasema tayari Wanyarwanda watano wameuwawa kinyama na kumekuwa pia na visa vya raia wa Rwanda kupotea, akiwemo mwandishi wa habari aliyetekwa nyara na hajawahi kuonekana tena. Mwanaharakati huyo anahisi maafisa wa ujasusi wa Rwanda ndio wanaohusika na utekaji nyara na mauaji hayo.

Kituo cha Nuvunga cha CDD sasa kinataka makubaliano yaliyotiwa saini kati ya marais wa Rwanda na Msumbiji wakati wa ziara ya Rais Kagame hivi majuzi mjini Cabo Delgado yawekwe wazi. Kulingana na taarifa iliyotolewa na shirika hilo la haki za binadamu, raia wa Msumbiji wana haki ya kufahamu kinachoendelea nchini mwao baada ya jeshi la Rwanda kuingia nchini humo na jinsi ushirikiano kati ya nchi hizo mbili unavyofanya kazi.