1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya mustakabali wa Libya matatani

9 Juni 2015

Bunge lililochaguliwa na wananchi Libya limekataa pendekezo la Umoja wa Mataifa la kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa, na kujiondoa katika mazungumzo yanayolenga kuumaliza mgogoro wa kugombea madaraka

Libyen Bürgerkrieg
Picha: Getty Images/AFP/M. Turkia

Hii ni baada ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa Bernardino Leon kusema kuwa pande zote mbili zimeichukulia kwa njia nzuri rasimu hiyo iliyowasilishwa baada ya mazungumzo ya Morocco hapo jana.

Leon amekitumia kipindi kizima cha leo asubuhi kufanya mashauriano na pande husika katika mgogoro wa Libya ili kusikia maoni yao kuhusiana na mkutano unaotarajiwa kuanza kesho mjini Berlin. Awali, Leon alisema pande zote hasimu zimeichukulia kwa njia nzuri rasimu ya makubaliano ya amani iliyopendekezwa katika mazungumzo yaliyokamilika jana nchini Morocco.

Huku akipata uungwaji mkono wa viongozi wa dunia, Leon anajaribu kushinikiza kupatikana makubaliano kabla ya kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan mnamo Juni 17. Hata hivyo ameonya kuwa hakuna muafaka utakaofanya kazi bila uungwaji mkono wa makundi yenye silaha nchini Libya.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Bernadino LeonPicha: Getty Images/AFP/Str

Wakiwa mjini Berlin, wajumbe wa serikali mbili hasimu za Libya wanatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Ulaya na nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Lakini akizungumza na shirika la habari la Reuters, mbunge mmoja wa Bunge la Libya lililochaguliwa na wananchi, Tareq al-Jouroushi amesema kuwa wameipinga rasimu hiyo ya Umoja wa Mataifa inayopendekeza kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa. Aidha amesema bunge limewapiga marufuku wajumbe wake kwenda Ujerumani hii leo kwa mazungumzo.

Washiriki wa mazungumzo hayo ni pamoja na wanachama wa serikali ya Libya inayotambulika kimataifa yenye makao yake mjini Tobruk, na wa kutoka serikali hasimu, muungano wa makundi ya wapiganaji wa Fajr ambao unaudhibiti mji wa Tripoli. Viongozi wa kundi la nchi saba zenye nguvu duniani wameziunga mkono juhudi za Leon za wakati wakiwataka viongozi wa Libya kuchukua maamuzi mazito ya kisiasa.

Rasimu hiyo ya makubaliano iliyowasilishwa jana ni ya nne, baada ya duru tatu za awali za mazungumzo kushindwa kufikia muafaka wowote.

Inapendekeza miongoni mwa mambo mengine kuundwa Serikali ya mpito ya Umoja wa Kitaifa kwa kipindi cha mwaka mmoja, na kisha kuongezwa muhula mwingine wa mwaka mmoja. Inaeleza kuwa bunge lililochaguliwa mwezi Juni, ambalo wabunge wengi wanaunga mkono serikali ya Tobruk, litachukua majukumu ya kutunga kisheria kw akipindi kizima cha mpito. Pia Baraza Kuu la Taifa litaundwa hasa kutoka kwa wanachama wa serikali pinzani ya Tripoli, ambalo litaelezea maoni kuhusiana na sheria zitakazotungwa.

Pande zote mbili zitayaleta pamoja makundi pinzani ya wapiganaji na kuunda jeshi jipya chini ya udhibiti wa moja kwa moja wa serikali ambapo wanajeshi wa zamani waasi watapewa fursa ya kujiunga au kuwarejesha katika maisha ya kiraia. Aidha rasimu hiyo inasema serikali ya umoja wa kitaifa kupitia taasisi zake mbalimbali za usalama, - jeshi na polisi – itachukua hatua mwafaka za kupambana na vitisho vya ugaidi nchini Libya.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri:Yusuf Saumu