1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi kuhusu uchaguzi nchini Palestina

Maja Dreyer4 Januari 2006

Ikiwa ni wiki tatu tu kabla ya kufanyika uchaguzi katika maeneo ya Wapalestina kuna mashaka yanayozidi ikiwa tarehe hiyo itaweza kutimizwa. Sababu ni kutokana na mashambulio yanayoendelea katika eneo la Gaza. Hiyo ndiyo moja ya mada zinazozingatiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

Mashambulio katika eneo la Gaza
Mashambulio katika eneo la GazaPicha: AP

Tuanze na mashambulio yanayoendelea kati ya Israel na Palestina. Gazeti la “Lausitzer Rundschau” la mjini Cottbus linachambua:

“Sio Waisraeli tu wanaosababisha uchaguzi wa Palestina usiweze kufanyika kwenye tarehe iliyopangwa. Sababu kuu ni hali ya ndani ya jamii ya Kipalestina, yaani kwanza mapambano ndani ya kundi la Fatah ambalo limegawanyika na linatumia silaha kupigana. Na pili ni udhaifu wa rais wa Palestina, Machmud Abbas, pamoja na taasisi zake na vyombo vya usalama. Bila ya uchaguzi, lakini, usalama hauwezi kuendelezwa, badala yake mashambulio yataongezeka.

Gazeti la “Landeszeitung” kutoka mjini Lüneburg lina shaka kwamba uchaguzi huo utaweza kuleta usalama. Wahariri wa gazeti hilo wanaandika:

“Kanuni moja ya wataalamu wa Kisiasa inasema: “Mataifa ya Kidemokrasia hayawezi kupigana vita”. Hata hivyo, hakuna uhakika kwamba uchaguzi utaleta usalama, kama matokeo ya eneo la Mashariki ya Kati yanavyoonyesha. Uchaguzi unayotarajiwa kufanyika katika eneo la Wapalestina na Israel unaongeza hatari ya vita. Kundi la vigogo wanaomzunguka rais wa Palestina Abbas ambalo zamani liliishi sana uhamishoni kwa sababu ya kisiasa, lilishindwa kuwatuliza wala kuungana na vijana waliokua katika kambi za wakimbizi na ambao ni wafuasi wa kundi la Hamas.

Ikiwa makundi ya Hamas na Islamic Dshihad yatashinda katika uchaguzi huo, tokeo kama hilo linamaanisha kutega baruti, kwani makundi yote mawili yanakataa Israel kuwa na haki ya kuwa taifa. Kwenye upande mwingine waziri mkuu wa Israel, Ariel Scharon, anaongeza mivutano baina na Israel na Palestina. Kinyume na amri yake ya Waisraeli kuondoka kutoka eneo la Gaza, sasa analishambulia eneo hilo pamoja na kuongeza makaazi ya Waisraeli katika ukingo wa Magharibi wa mto Jordan.”

Hali ya usalama nchini Ufaransa

Na kwa mada nyingine: Mwanzo mwa wiki, rais wa Ufaransa, Jacques Chiras, alisema sheria ya hali ya hatari iliyotangazwa wakati wa ghasia nchini humo mnamo mwezi Novemba itaondolewa. Kuhusu swala hilo, gazeti la Frankfurter Rundschau lina maoni yafuatayo:

“Kwa kweli kuna usalama nchini humo ambamo katika mkesha wa wa mwaka mpya magari 425 yalitiwa moto na polisi 27 walijeruhiwa? Inamaanisha nini kuhusu hali ya jamii kama maprofesa wachache tu walipinga sheria ya hali ya hatari kutangazwa lakini jamii kwa jumla inakaa kimya? Inamaanaishi nini, hasa kwa nchi kama hiyo ambayo inapenda kuyafahamisha mataifa mengine juu ya mambo kama haki za binadamu au uhuru wa wananchi? Ghasia nchini Ufaransa zinafichua mifarakano ya jamhuri inayosifu matamshi yake makubwa, kama vile: “Uhuru, Usawa na Undugu” lakini ambapo wakaazi wa mitaa maskini hubaguliwa na huwekwa kando mwa jamii.”

Ajali ya jengo la michezi ya barafuni nchini Ujerumani

Na kutoka Ufaransa mwishoni tunaelekea Ujerumani ambapo hivi juzi watu 12 waliuawa baada ya jumba la michezo la barafuni liliporomoka. Ajali hiyo iliwasababisha wahariri wa magazeti kuzikosoa taratibu za kiserikali za kuchunguza usalama wa majengo ya serikali. Gazeti la “Kölner Express” kutoka Cologne linaandika:

“Kila gari au ndege inachunguzwa mara kwa mara baada ya kipindi cha miaka fulani. Lakini kuhusu majengo ya michezo au shule ambapo tunataka kupumzika au watoto wanatarajiwa kujifunza bila ya kujali mambo mengine hakuna sheria inayosema ni lazima majengo hayo yachunguzwe. Je, inabidi kufahamu utata huo? Hapana! Tunahitaji sheria kama hiyo!”

Gazeti la EßLINGER ZEITUNG, linaeleza kwa nini jambo hili litakuwa gumu zaidi.

Uwezekano wa kuwepo ulegevu na makosa utajulikana mara tu matokeo ya uchunguzi wa kina yatakapotangazwa. Hata hivyo inajulikana kufikia leo hii kwamba ajali iliyotokea mjini Bad Reichenhall ni tukio lililosababisha wasiwasi. Katika jamii nyingi za hapa Ujerumani kuna majengo mengi yanayohitaji kufanyiwa ukarabati; ziwe ni shule, mabwawa ya kuogelea, majumba ya maonyesho na mikutano au majumba mengine. Mara nyingi miji na tawala za mikoa ambazo zinakabiliwa na changamoto kubwa kifedha haziwezi tena siku hizi kugharimia shughuli ya ukarabati wa majengo.