Wasiwasi Uganda siku moja kabla ya Rais Museveni kuapishwa
11 Mei 2021Polisi wanadai kuwa hizi ni miongoni mwa njama za upinzani kuvuruga amani wakati wa kuapishwa kwa rais Yoweri Museveni hapo kesho. Lakini upinzani unapinga kabisa madai hayo na kuyataja kuwa hila za vyombo vya usalama kutaka kupewa pesa na serikali kushughulikia hali ambayo inatokana na taarifa za kupotosha.
Soma pia: Wafuasi 40 wa Bobi WIne wakamatwa Uganda kwa kuandamana
Visa kadhaa vya watu wasiojulikana wanaodaiwa kusafiria kwenye pikipiki kurusha mabomu ya petroli vimeripotiwa tangu hapo jana. Visa hivyo ambavyo vimeukumba hasa mji wa Kampala siku moja kabla ya kuapishwa kwa Rais Yoweri Museveni kwa awamu ya sita vimeelezewa na polisi kuwa miongoni mwa mipango ya upinzani kuvuruga shehere hizo.
Hadi sasa hakuna mtu ametajwa kupoteza maisha wala kujeruhiwa katika visa hivyo. Ila upande wa upinzani hususan cha cha NUP umekanusha vikali madai hayo pamoja na yale kuwa aliyekuwa mgombea urais Robert Kyagulanyi amepangiwa kuapishwa kama rais na wafuasi wake.
Viongozi wa NUP wamesisitiza kuwa hawana mipango yoyote ya kumwapisha kiongozi wao maarufu kama Bobi Wine kwenye wadhifa wa urais kama uvumi unavyoenezwa na vyombo vya usalama.
Mnamo Jumatatu, askari wa vyombo vya usalama walizingira makazi ya viongozi wa upinzani Bobi Wine pamoja Dkt. Kiiza Besigye katika kile ambacho polisi wamesema ni hatua ya kuwadhibiti wasiendeshe shughuli zozote za kutatiza kuapishwa kwa rais Museveni siku ya Jumatano.
Hata hivyo haijafahamika kama viongozi hao wamo kwenye makazi yao.