1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi wa kurejea kwa kundi la Mungiki nchini Kenya

23 Novemba 2023

Wabunge wanawake nchini Kenya wameelezea hofu kuhusu kuibuka tena kwa kundi haramu la Mungiki wakiitaka serikali kuwachunguza viongozi wanaohusishwa na kundi hilo.

DW Videostill | Kenia Binnenflüchtlinge
Watu wakikimbia vurugu za baada ya uchaguzi nchini KenyaPicha: DW

Kundi la Mungiki ambalo liliwahangaisha wananchi kwa muda mrefu, liliangamizwa zaidi ya miaka kumi na nne iliyopita. Aliyekuwa kiongozi wa Mungiki Maina Njenga amekuwa mjini Nakuru kwa siku mbili kufuatilia kesi yake inayoendelea katika mahakama ya Nakuru, ambapo ameshtakiwa kwa kuhusika na kundi hilo. Maafisa wa usalama walionekana kwa wingi wakishika doria mjini na katika lango la mahakama, huku umati mkubwa wa wafuasi wa Maina Njenga ukiandamana naye ambapo alizungumza nao.

Maina Njenga anaaminika kujitafutia umaarufu eneo la Mlima Kenya kama kiongozi wa jamii hiyo, nafasi ambayo pia inawaniwa na naibu Rais Rigathi Gachagua. Lakini mikutano hii inaibua hofu katika baadhi ya maeneo nchini. Viongozi wanawake kutoka eneo la Mlima Kenya wanasema watu wanapowaona viongozi wanaohusishwa na kundi haramu la Mungiki wakishabikiwa na umma pamoja wanafikwa na hofu.

Wazo la kuchunguzwa kwa viongozi wa Mungiki

Wafuasi wa vyama vya siasa wakisiliza mgombea urais Raila Odinga wakati wa kampeni za uchaguzi uliopitaPicha: Luis Tato/AFP

Anne Muratha, mbunge wa kiambua anasema viongozi wanaohusishwa na kundi hilo wanapaswa kuchunguzwa na hatua kali kuchukuliwa. Viongozi hao wa kike wamesema unyama waliotekeleza Mungiki maeneo ya kati, Nairobi, na bonde la ufa haujasahaulika. Mbunge wa Thika Alice Ng'ang'a anaeleza kuwa wazazi wameanza kuogopa kwamba watoto wao wa kiume wataanza kulazimishwa kujisajili kuwa wafusasi wa kundi hilo haramu.

Soma zaidi:Malumbano baina ya Mungiki na Polisi wa Kenya

Anaitaka serikali kuchukua hatua za haraka kuzuia kuchipuka tena kwa kundi hilo. Mwaka 2007 aliyekuwa Waziri wa usalama wa ndani John Michuki alianza oparesheni ya kuliangamiza kundi haramu la Mungiki. Hata hivyo mafanikio ya oparesheni hiyo yaliibua shutma za polisi kuua na kuchukua hatua kupita kiasi, na hata kupelekea ujumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kutumwa nchini kuchunguza madai hayo.  

DW, Nakuru

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW