1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaLebanon

Wasiwasi wa kuzuka vita kamili kati ya Hezbollah na Israel

2 Februari 2024

Matarajio ya vita kamili kati ya Israel na Hezbollah yanawatia hofu watu wa pande zote mbili za mpaka, lakini wengine wanauona kama mzozo usioepukika kutokana na vita vya Israel vinavyoendelea dhidi ya Hamas.

Wanamgambo wa Kishia wa Iraq Kataib Hezbollah
Wanamgambo wa Kishia wa Iraq Kataib HezbollahPicha: dpa/picture alliance

Vita kama hivyo vinaweza kusababisha madhara makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa na upande wowote. Iddi Ssessanga anaangazia kitisho juu ya vita hivyo katika ripto ifuatayo.

Israel na Hezbollah zina funzo kutokana na vita vyao vya mwisho, vilivyotokea mwaka 2006, vilivyodumu kwa mwezi mzima na kumalizika kwa kile wadadisi wa mambo walichokiita sare. Pia wamekuwa na miezi minne ya kujiandaa kwa vita vingine, licha ya juhudi za Marekani kuzuia kuenea kwa mzozo kati ya Israel na Hamas.

Vita vya 2006, miaka sita baada ya majeshi ya Israel kuondoka kusini mwa Lebanon, vilizuka baada ya Hezbollah kuwakamata wanajeshi wawili wa Israel na kuwaua wengine kadhaa katika shambulio la kuvuka mpaka. Israel ilianzisha mashambulizi ya anga na ardhini na kuweka kizuizi ambacho kililenga kuwakomboa mateka na kuharibu uwezo wa kijeshi wa Hezbollah, katika oepresheni ambayo hatimaye ilishindwa.

Soma pia: Kundi la Hezbollah lashambulia kamandi ya kijeshi ya Israel

Mashambulizi ya Israel yalisawazisha maeneo makubwa ya Lebanon kusini na vitongoji vya kusini mwa Beirut, huku Hezbollah ikirusha maelfu ya maroketi yasioongozwa kuelekea jamii za kaskazini mwa Israeli.

Mzozo huo uliua Walebanon 1,200, wengi wao wakiwa raia, na Waisraeli 160, wengi wao wakiwa wanajeshi. Azimio la Umoja wa Mataifa lililohitimisha vita hivyo lilitoa wito wa kuondolewa kwa vikosi vya Israel nchiniLebanon na kuundwa kwa eneo lisilo na shughuli za kijeshi kwenye upande wa mpaka wa Lebanon.

Licha ya kupelekwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, Hezbollah inaendelea kuendesha shughuli zake katika eneo la mpakani, huku Lebanon ikisema Israel inakiuka mara kwa mara mamlaka ya anga yake na inaendelea kukalia maeneo ya ardhi ya Lebanon. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alionya mwezi uliyopita kuwa vita kati ya Israel na Hezbollah vitakuwa janga kamili, katikati mwa msusuru wa diplomasia ya Marekani na Ulaya.

Hakuna upande wowote unaoonekana kutaka vita

Mwanajeshi wa Israel aliyevaa kiraka nyuma ya koti lake lenye picha ya kiongozi wa Hezbollah Hassan NasrallahPicha: Jalaa Marey/AFP/Getty Images

Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah hajatishia kuanzisha vita lakini alionya kuhusu mapambano yasio na kikomo, ikiwa Israel itafanya hivyo.

Hezbollah inasema haitakubali kusitishwa kwa mapigano kwenye mpaka wa Israel-Lebanon kabla ya usitishwaji huo kutokea Gaza na imepinga pendekezo la Marekani la kuhamisha vikosi vyake kilomita kadhaa nyuma kutoka mpakani, kulingana na maafisa wa Lebanon.

Licha ya matamshi makali kutoka pande zote, hakuna upande unaoonekana kutaka vita, anasema Andrea Teneti, msemaji wa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kusini mwa Lebanon, na kuongeza hata hivyo kwamba makosa ya kihesabu yanaweza kusababisha mzozo mpana ambao ungekuwa mgumu sana kudhibitiwa.

Hezbollah na jeshi la Israeli wamepanua uwezo tangu 2006, lakini nchi zote mbili pia ni dhaifu zaidi, anasema Teneti.

Mzozo wa kiuchumi wadhoofisha taasisi za umma Lebanon

Mwanamke akitembea kati ya vifusi vya jengo lililoharibiwa na shambulio la anga la Israel huko Naqoura, Lebanon.Picha: Ali Hashisho/Xinhua/picture alliance

Nchini Lebanon, miaka minne ya mgogoro wa kiuchumi imedhoofisha taasisi za umma, ikiwa ni pamoja na jeshi lake na gridi ya umeme, na kuharibu mfumo wake wa afya.

Nchi hiyo inayohifadhi zaidi ya wakimbizi milioni 1 wa Syria, ilipitisha mpango wa dharura wa hali ya vita mwishoni mwa Oktoba, ikikadiria Waleboni milioni 1 wataihama nchi yao katika muda wa siku 45.

Soma pia: Borell aonya Lebanon kuingizwa vitani Mashariki ya Kati

Israel inahisi matatizo ya kiuchumi na kijamii kutokana na vita vya Gaza, ambavyo vinatarajiwa kugharimu zaidi ya dola bilioni 50, au takriban asilimia 10 ya shughuli za kiuchumi za kitaifa hadi mwisho wa 2024, kulingana na Benki ya Israel. Gharama zinatazamiwa kupanda sana ikiwa kutakuwa na vita na Lebanon.

Vita kamili vinaweza kuenea na kuhusisha pande nyingi, yakiwemo makundi ya uwakala wa Irani nchini Syria, Iraqi na Yemeni, na yumkini kuiingiza hata Iran yenyewe. Vinaweza pia kuivuta Marekani, mshirika wa karibu wa Israel, zaidi katika mzozo huo, ambayo tayari imetuma imetuma meli za ziada za kivita katika eneo hilo.