1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ECOWAS yapitisha kupeleka jeshi Niger

11 Agosti 2023

Mvutano kati ya watawala wa kijeshi na jumuiya ya ECOWAS waongezeka baada ya taasisi hiyo kuamua jeshi lake la dharura lipelekwe Niger kurudisha utawala wa kikatiba

Nigeria Abuja | ECOWAS-Treffen zu Niger-Putsch
Viongozi wa ECOWAS waliokutana AbujaPicha: Gbemiga Olamikan/AP/picture alliance

Mivutano inaongezeka kati ya watawala wapya wa kijeshi wa Niger na jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS baada ya jumuiya hiyo kupitisha uwamuzi jana usiku wa kutuma jeshi lake la dharura kurudisha utawala wa kidemokrasia Niger. 

Usiku wa kuamkia leo Ijumaa, Jumuiya ya ECOWAS ilitangaza msimamo wake kwamba imeshatowa maagizo ya kupelekwa kile ilichokiita kikosi cha dharura kurudisha utawala wa kikatiba nchini Niger baada ya muda wa hadi Jumapili iliyopita,iliyoutowa wa kurudishwa madarakani rais Bazoum kupita bila ya hatua hiyo kuchukuliwa.Tangazo hilo lilitolewa katika mkutano wa kilele mjini Abuja na rais wa tume ya ECOWAS Omar Touray.

"Mamlaka ya ECOWAS inatowa maagizo kwa kamati ya wakuu wa majeshi kukiweka tayari kikosi cha dharura cha ECOWAS kwa ukamilifu wake mara moja. Viongozi wameweka wazi kwamba wamechukua uamuzi huu kufanya wajibu wao na kwa mujibu wa mipango na azma yao. Haina maana kwamba wanakinyongo dhidi ya nchi yoyote au mtu yoyote.Huu ni msimamo wa kikanda''

 

Soma Pia: Maelfu ya watu waandamana Niger kupinga vikwazo vya ECOWAS

Jumuiya hiyo imeendelea pia kulaani hatua ya kushikiliwa kwa rais Mohammed Bazoum,familia yake na maafisa wa serikali yake. Saa kadhaa kabla ya uamuzi huu wa ECOWAS maafisa wawili kutoka nchi za Magharibi waliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba jeshi la Niger lilimwambia mwanadiplomasia wa ngazi za Juu wa Marekani kwamba watamuua rais Bazoum ikiwa nchi jirani zitajaribu kuingilia kijeshi kuurudisha utawala wake.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akiwa na rais wa Niger,Mohammed Bazoum March 16 kabla ya kupinduliwa madarakaniPicha: Boureima Hama/AFP/Getty Images

Umoja wa Ulaya umesisitiza wasiwasi wake kuhusu mazinngira anayozuiliwa rais Bazoum na Familia yake. Lakini pia waziri wa mambo ya nje wa Marekani ambayo imeiunga mkono ECOWAS, Antony Blinken naye pia alisema wana wasiwasi na hali ya Bazoum.

''Tuna wasiwasi mkubwa  juu yake na familia yake kuhusu usalama wake na ustawi wake. Pia tumeweka wazi kwa viongozi wa kijeshi kwamba tutawabebesha dhamana wao ya usalama na afya yake.''

Kutumwa kwa Jeshi la ECOWAS

Hata hivyo mpaka sasa bado haijafahamika waziwazi lini au wapi hasa kikosi cha ECOWAS  kitatumwa  na nchi zipi kati ya wanachama wake 15 zitachangia kwenye jeshi hilo. Taarifa za wataalamu zinasema jeshi hilo huenda likawa na askari kiasi 5000 watakaoongozwa na Nigeria na inawezekana likawa tayari kutumwa ndani ya wiki chache.Soma pia: ECOWAS bado inatumai kuna fursa ya upatanishi Niger

Baada ya mkutano wa jana rais wa nchi jirani ya Ivory Coast Allassane Outtara alisema nchi yake itashiriki kwenye operesheni hiyo dhidi ya Niger,msimamo ambao pia umechukuliwa na Nigeria na Benin.Waniger wanaikosoa hatua ya ECOWAS wakiita ni kitendo cha uchokozi. Mwanaharakati wa mashirika ya kiraia Ibrahim Bana anasema

Raia wa Niger wakiwasaidia wanajeshi mjini Niamey baada ya mapinduzi Julai 30Picha: AFP/Getty Images

Tunapaswa kuuita uuingiliaji huu wa kijeshi kama ulivyo,ni uchokozi dhidi ya watu wetu.Hakuna sheria yoyote ya  ECOWAS inayowapa mamlaka viongozi wa nchi kuamuwa kupeleka jeshi katika nchi yoyote mwanachama,kwa sababu yoyote ile.Hiki ni kitendo cha kimabavu.'''

Jeshi la Niger lilifanya mapinduzi Julai 26 yakiwa ni mapinduzi ya saba kutokea katika ukanda wa Magharibi mwa Afrika na Afrika ya Kati katika kipindi cha miaka mitatu.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri; Bruce Amani

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW