Wasiwasi waongezeka huko Kivu wakati mazungumzo yakiendelea
24 Oktoba 2025
Kutokea Goma, viongozi wa kundi la AFC/M23 wamelaani kile wanachokiita "uvunjaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya kusitisha vita" unaofanywa na Jeshi la Taifa la Kongo (FARDC) pamoja na washirika wake.
Wamesema maeneo kadhaa waliyokuwa wakiyadhibiti yameshambuliwa kwa mabomu katika wilaya za Walikale, Masisi na Kalehe, ikiwemo kiwanda cha uchimbaji dhahabu cha Twangiza, ambacho kimeripotiwa kushambuliwa mara mbili mwezi Oktoba.
Corneille Nangaa, mratibu wa kisiasa wa kundi hilo, ameitaja hatua hiyo kuwa "uhalifu dhidi ya amani" na akaishutumu serikali ya Kinshasa kwa kuvuruga juhudi za kidiplomasia zinazoendelea mjini Doha na Washington. Hata hivyo, wakaazi wa Goma wanasema wanaishi kwa hofu kubwa ya kurejea kwa mapigano.
"Mimi kama mkazi wa Goma na mmoja wa waathirika wa uzembe wa serikali ya Kinshasa, jana nilisikia viongozi wa kundi hilo wakitishia kujibu mashambulizi. Makundi haya mawili yalikubaliana kuketi meza ya mazungumzo kule Doha, lakini ndiyo hao hao wanaokiuka makubaliano ya kusitisha mapigano. Ni sisi wananchi tunaendelea kuwa waathirika wa vitendo vyao. Maelfu waliuawa wakati wa kupokonywa kwa mji wa Goma, sasa mtu anaweza kujiuliza, wanawezaje tena kutangaza vita?", alihoji mkaazi huyo.
"Kila upande unataka kudhihirisha kwamba wao wako sahihi"
Kwa upande wa serikali, msemaji wake amekanusha madai ya mashambulizi hayo, akiyataja kama "uzushi wa waasi.” Lakini kwa wanaharakati wa kijamii, pande zote mbili zinajionyesha kama wahanga kwenye mitandao ya kijamii, huku wananchi wa kawaida wakiendelea kubeba mzigo wa mateso.
Mmoja wa wanaharakati hao, ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema kuwa bado njia ni ndefu kufikia mani huko Mashariki mwa Kongo.
"Ni wananchi ndio wanaoendelea kuwa waathirika wa hali inayoendelea nchini. Amani inapaswa kuletwa na pande zote mbili. AFC/M23 inataka kuonyesha ulimwenguni kwamba inataka amani, na serikali ya Kongo nayo inadai hivyo. Lakini kila upande unataka kudhihirisha kwamba wao wako sahihi. Kama kweli wangetaka amani, mazungumzo ya Doha na Washington yangekuwa ya dhati na yenye matokeo", alisema mwanaharakati huyo.
Watu milioni 21 wahitaji msaada wa kibinadamu
Kwa mujibu wa shirika la misaada Oxfam France, zaidi ya Wakongo milioni 21 wanahitaji msaada wa dharura, huku zaidi ya milioni 28 wakikabiliwa na njaa.
Hospitali zimeelemewa, barabara zimeharibiwa, na inakadiriwa kuwa mwanamke mmoja hubakwa kila baada ya dakika nne. Licha ya ukubwa wa janga hilo, ufadhili wa misaada ya kibinadamu umepungua kwa takriban theluthi mbili ndani ya mwaka mmoja.
Oxfam inatoa wito kwa mkutano wa kimataifa kuhusu Maziwa Makuu, unaotarajiwa kufanyika nchini Ufaransa tarehe 30 Oktoba, kuchukua hatua madhubuti badala ya kutoa maneno matupu, ili kufufua mchakato wa amani mashariki mwa Kongo.