1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasomali waliozaliwa Uganda sasa kutambuliwa kisheria

Lubega Emmanuel24 Machi 2022

Mahakama Kuu nchini Uganda imeagiza kwamba watu wenye asili ya Kisomali waliozaliwa nchini humo au kuwa na uhusiano wa ndoa na wenyeji watambuliwe kisheria kama raia.

Somalische Stammesführer in Uganda
Picha: Simone Schlindwein

Maagizo haya yamepokelewa kwa furaha na jamii zingine zinazokabiliwa na hali hiyo ya kubaguliwa ikiwemo Wahindi, Waarabu, Wanubbi na Wanyarwanda.

Watu wenye asili ya Kihindi, Kiarabu, Kinubi, Kinyarwanda pamoja na Kisomali hupata matatizo makubwa wakati wanapohitaji kupata vitambulisho vya uraia nchini Uganda na vibali vya usafiri. Hii ni kwa sababu si rahisi kubaini kama mhusika alizaliwa Uganda au ana uhusiano wa ndoa au uzazi na yule ambaye anatambuliwa kisheria kuwa raia. Katika hali hii, watu wengi wa jamii hizo hujikuta wakibaguliwa ikidaiwa kuwa wao ni wageni.Mkutano kuhusu Somalia wafanyika Kampala

Lakini sasa mahakama kuu imetoa mwelekeo ambao umewaletea nafuu na furaha. Hii ni kutokana na shauri lililowasilishwa na kundi moja la watu wenye asili ya Kisomali. Mmoja kati ya waliowasilisha shauri hilo ni mwenyekiti wa jamii ya Wasomali nchini Uganda.

Wasomali nchini UgandaPicha: Simone Schlindwein

Katika kutoa maamuzi hayo, Jaji Musa Sekana ametoa angalizo kuwa mwendelezo wa kuwanyima watu hao vitambulisho vya uraia ni sawa na kudai kuwa hawana utaifa wowote duniani kwani sheria za kimataifa na hata katiba ya Uganda zimeweka bayana suala la uraia wa watu wasio wa asili ya nchi, lakini walihamia nchini miaka kadhaa iliyopita. Hata hivyo kuna baadhi ya wenyeji wa Uganda wanaopinga hatua ya kuzitambua jamii zisizo na asili ya nchi hiyo kutambuliwa kama raia.

Lakini pia kuna wenyeji wanaounga mkono haki ya watu wasio wenye asili ya Uganda kutambuliwa rasmi kama raia. Wana mtazamo kuwa watu wenye asili ya Kihindi, Kiarabu, Kisomali na kadhalika wametoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi. Ken Lukwago ni mchambuzi wa masula ya kijamii.

Mara kwa mara mjadala huibuka kuhusu suala la kurasimisha uraia wa watu wenye asili za kigeni, lakini ambao idadi ya ni kubwa. Viongozi wa jamii hizo wameshuhudiwa mara kadhaa wakitoa rai kwa serikali iwatambue na kuwaondolea kero ya kubaguliwa. Wale wa Kihindi hata wapendekeza watambuliwe kama mojawapo ya makabila ya Uganda. Wale wenye asili ya Kinyarwanda walifikia hatua ya kutaka kubadili utambulisho wao waiitwe Bavandimwe.