1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Wasudan waadhimisha Eid al-Adha katikati mwa mapigano

Sylvia Mwehozi
29 Juni 2023

Mamia ya waumini wa Kiislamu mjini Khartoum walikusanyika jana kuombea amani ya nchi yao katika siku ya kwanza ya sikukuu ya Eid al Adha, huku baadhi ya raia wakiripoti milio ya risasi katika viunga vya mji huo.

Sudan Eid al-Fitr
Waumini wa Kiislamu wa Sudan wakiadhimisha sikukuu ya Eid al-fitr Aprili 2023Picha: AFP

Mashuhuda katika mji pacha wa Omdurman, wameripoti mashambulizi ya anga na milio ya kuzuia ndege za kivita, licha ya makubaliano tofauti ya upande mmoja yaliyotangazwa na majenerali wanaopigana kwa ajili ya sikukuu ya Eid al Adha. Waumini wa Kiislamu nchini humo walikusanyika ili kusali, kukumbatiana na kutakiana heri katika kipindi cha muda mfupi cha kupumzika na milio ya risasi ya zaidi ya wiki 10, mashambulizi ya anga na mizinga ambayo imeharibu makaazi yao. Mikusanyiko kama hiyo ilifanyika nje ya Khartoum, ikiwa ni pamoja na mkoa wa Jazira ambapo watu wengi wamekimbilia kutoka mji mkuu.

Wasudan waendelea kushambuliana licha ya makubaliano

Katika hotuba yake ya Eid kiongozi wa jeshi wa Sudan Abdel Fattah al-Burhan alitoa wito kwa "vijana wa Sudan na wale wote wenye uwezo" kujiunga na jeshi ili kuitetea nchi. Wito kama huo ulitolewa na wizara ya ulinzi mwezi uliopita, lakini unaonekana kukataliwa pakubwa na raia. Burhan alisema kuwa, "hali hii inamtaka kila mtu kuwa tayari kukabiliana na mambo yanayotokea katika taifa letu. Vijana wote na wale wanaoweza kuitetea, wasisite au kuchelewa kutekeleza jukumu hili la kizalendo katika makaazi yao au kwa kujiunga na vitengo vya kijeshi."

Waumini wa Kiislamu wa Sudan wakiadhimisha sikukuu ya Eid al-fitr mapema mwaka huuPicha: AFP

Takriban watu 2,800 wameuawa na zaidi ya milioni 2.8 wamekimbia makaazi yao katika mapigano kati ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo, ambaye anaongoza kikosi cha msaada wa dharura cha RSF. Makubaliano tofauti ya kusitisha mapigano yaliyotangazwa kipindi cha nyuma na pande zote mbili yamekuwa yakikiukwa  mara kwa mara. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan UNITAMS ulikaribisha tangazo la makubaliano tofauti ya upande mmoja ya kusitisha mapigano, ukisema "Sikukuu ya Eid al-Adha iwe ukumbusho kwamba mapigano lazima yakome."

Kulingana na Umoja wa Mataifa, Waislamu wengi wa Sudan wangeweza kumudu gharama ya kuchinja mnyama kwa ajili ya Eid katika kipindi cha nyuma, lakini sasa watu milioni 25 nchini humo wanahitaji misaada ya kibinadamu.

Na huko katika eneo la magharibi la Darfur hali inaendelea kuwa mbaya zaidi.Umoja wa Mataifa unasema miji yote imezingirwa na vitongoji vimeteketezwa kabisa. Wakaazi, Umoja wa Mataifa, Marekani na wadau wengine, wanasema raia wamekuwa wakilengwa na kuuawa kutokana na makabila yao.Mauaji hayo yanadaiwa kufanywa na kundi la wanamgambo la RSF na washirika wao wapiganaji wa kiarabu.

Chanzo:afp