1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasudan waendelea kushambuliana licha ya makubaliano

21 Juni 2023

Mapigano makali yamezuka tena wenye mji mkuu wa Sudan, Kahrtoum mapema leo wakati masaa 72 ya makubaliano ya kusitisha mapigano yakifikia mwisho, makubaliano ambayo, hata hivyo, yalikuwa yakivunjwa mara kwa mara.

Sudan Khartum | Rauch und Flammen in Omdurman
Picha: REUTERS

Kwa mujibu wa mashahidi, muda mchache kabla ya muda wa mwisho wa makubaliano hayo kufika, majira ya saa 12:00 asubuhi ya Jumatano (Juni 21), mapigano yalizuka kwenye miji yote miji yote mitatu inayouzunguka Mto Nile: Khartoum, Bahri na Omdurman.

Ndege za kijeshi zilishambulia kwenye mji wa Bahri, ambako vikosi vya RSF vilijibiza mashambulizi hayo kwa kufyatua makombora ya kutungulia ndege.

Soma zaidi: Jeshi laonya hali ya hatari Sudan baada ya kikosi cha kutuliza ghasia kupelekwa mitaani

Milio ya makombora na risasi imesikika pia kwenye mji wa Omdurman, na kusini mwa mji mkuu, Khartoum, kulitokea mapigano ya waziwazi. 

Mashahidi pia wameripoti makabiliano ya ana kwa ana katika kambi moja ya jeshi kwenye jimbo la Kordofan ya Kusini, ambako kundi moja kubwa la waasi lisilofahamika upande linaoegemea kati ya jeshi la serikali na RSF limekuwa likijikusanya.

Kuvunjwa makubaliano

Makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yalikuwa mojawapo tu kati ya makubaliano mengi ya aina hiyo yaliyosimamiwa na Saudi Arabia na Marekani kwenye mazungumzo ya Jeddah.

Moto ukizuka baada ya mashambulizi ya angani kusini mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum.Picha: Altaher Hassan Ibn Awf/REUTERS

Lakini kama yalivyokuwa ya awali, na haya nayo yalikuwa yakivunjwa mara kwa mara na pande zote mbili, huku kila upande ukitupa shutuma kwa mwengine kwa kuanza kuyavunja.

Soma zaidi: Raia kadhaa wa Sudan wameuwawa kwa kushambuliwa au kupigwa risasi wakati wakajaribu kuukimbia mji wa El Geneina

Jioni ya jana, mahasimu hao walitupiana lawama kwa moto mkubwa uliozuka kwenye jengo la makao makuu ya idara ya ujasusi, ambalo limo ndani ya eneo la eneo la wizara ya ulinzi linalowaniwa tangu mapigano yaanze Aprili 15.

Marekani na Saudi Arabia zimesema ikiwa mahasimu hao wataendelea kushindwa kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano, zitafikiria kuyasitisha majadiliano yanayoendelea mjini Jeddah, ambayo, hata hivyo, wachambuzi wanasema hayana ufanisi wowote.

Kuwania madaraka

Mapigano yaliripuka nchini Sudan kutokana na mabishano juu ya mpango unaoungwa mkono kimataifa wa kuwa na kipindi cha mpito kuachana na utawala wa kijeshi kuelekea wa kiraia.

Mahasimu wa Sudan: Abdul Fattah Al-Burhan (kushoto) na Mohamed Hamdan Dagalo.Picha: Bandar Algaloud/Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Mpango huo ulibuniwa kufuatia mapinduzi ya kijeshi mwaka 2021 na miaka minne baada ya vuguvugu la umma kumng'oa madarakani mtawala wa muda mrefu, Omar Hassan al-Bashir.

Soma zaidi: Idadi ya wakimbizi wa Sudan yavuka nusu milioni

Jeshi rasmi la Sudan chini ya Jenerali Abdel-Fattah Burhan na Kikosi cha Dharura cha RSF chini ya Mohamed Hamdan Dagalo wamekuwa wakipambana kwa zaidi ya miezi miwili kuwania udhibiti wa madaraka, wakitumia silaha nzito nzito ambazo zimezigeuza baadhi ya sehemu za miji mikubwa nchini humo kuwa magofu.  

Mapambano yao yamechochea ghasia kusambaa kwenye jimbo la magharibi la Darfur na kusababisha zaidi ya watu milioni 2.5 kukimbia nchi.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW