1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataalam wa UN waeleza jinsi Rwanda imehusika na mzozo DRC

23 Desemba 2022

Wataalam huru wa Umoja wa Mataifa wamesema jeshi la Rwanda lilihusika kwenye ‘operesheni za kijeshi‘ dhidi ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika maeneo yanayokumbwa na machafuko mashariki mwa Congo.

DR Congo Kongolesische Jugendliche schließen sich der Armee an, um Rebellen zu bekämpfen
Picha: Benjamin Kasembe/DW

Kulingana na ripoti ya wataalam hao ambayo shirika la habari la AFP limepata nakala yake, kuna ushahidi wa kutosha kwamba jeshi la Rwanda liliingilia kati moja kwa moja katika vita vya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo dhidi ya waasi wa kundi la M23, na kwamba jeshi hilo liliwaunga mkono waasi hao kwa kuwapa silaha, risasi na magwanda au sare za kivita.

Rwanda yadai mauaji ya Kishishe ni ya kutungwa na DRC

Ripoti hiyo inajiri mnamo wakati Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa ikiishutumu Rwanda kwa kuliunga mkono kundi la M23.

Msemaji wa serikali mjini Kigali alikanusha madai kwamba Rwanda iliwaunga mkono waasi wa M23. Aidha alikataa kuzungumzia tuhuma nyinginezo dhidi ya Rwanda hadi pale ripoti hiyo ilipochapishwa rasmi.

Tangu mwishoni mwa mwaka uliopita, wanamgambo wa kundi hilo wamekamata sehemu kubwa za maeneo yanayokumbwa na machafuko ya mashariki mwa Congo.

Mapigano kati ya jeshi la Jamhuri ya Congo na waasi wa M23 yamekaribia mji wa kibiashara Goma.Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Mapigano yakaribia mji wa Goma

Imeripotiwa mapigano kwa sasa yamesogea karibu sana na mji wa kibiashara Goma umbali wa takriban kilomita 21 kutoka mji huo ulio na zaidi ya wakaazi milioni moja.

Rwanda imekuwa ikikana kuwaunga mkono waasi hao. Lakini Marekani, Ufaransa miongoni mwa mataifa mengine ya Magharibi wanakubaliana na tuhuma za Congo.

Je viongozi wa Afrika wanatosha kusuluhisha migogoro yao?

Kulingana na ripoti hiyo ya wataalam wa Umoja wa Mataifa, jeshi la Rwanda liliingilia kati kwa kuimarisha vikosi vya M23, na vilevile kupambana na kikosi cha Kidemokrasia cha Ukombozi wa Rwanda, ambacho ni sehemu ya vikundi vya Wahutu wenye itikadi kali wa Rwanda waliotekeleza mauaji ya kimbari ya Watutsi mwaka 1994 nchini Rwanda.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa Rwanda iliwaimarisha wanamgambo wa M23 kwenye operesheni maalum hususan zilizolenga kukamata miji na maeneo ya kimkakati.

Mzozo wa kivita mashairki mwa DR Congo; ni ipi suluhu?

This browser does not support the audio element.

Wataalam wasema Rwanda iliongoza mashambulizi ya pamoja na M23

Kulingana na ripoti hiyo, wanajeshi wa Rwanda pia waliongoza mashambulizi ya pamoja na wanamgambo wa M23 dhidi ya maeneo ya wanajeshi wa Congo mnamo mwezi Mei.

Ripoti hiyo yenye kurasa 236 itakayokabidhiwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, inatarajiwa kuchapishwa rasmi siku chache zijazo.

Malumbano yaendelea baina ya Kongo na Rwanda

Alain Mukuralinda, naibu msemaji wa serikali ya Rwanda alisema serikali yake haijaona kiini cha ripoti hiyo au ushahidi uliotokana nao.

"Leo hii, maadamu hatujaona Ushahidi, na maadamu hatujachunguza hicho kinachotajwa kuwa ushahidi, ni vigumu kuchukua msimamo,” aliliambia shirika la habari la AFP. Lakini aliongeza kuwa hawaungi mkono kundi la M23, wala hawalihitaji kundi hilo.

Chanzo: AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW