1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Maji machafu ya ndege za China kupimwa kugundua virusi

5 Januari 2023

Mataifa kadhaa duniani yanasema yatachunguza maji machafu ya ndege zinazoruka kutokea China ili kujuwa kiwango cha maambukizo ya UVIKO-19 na endapo kuna aina mpya za virusi hivyo katika taifa hilo la Asia.

Mehr Länder führen Corona-Testpflicht für Reisende aus China ein
Picha: Danny Lawson/PA Wire/dpa/picture alliance

Upimaji huo unahusu mchanganyiko wa mkojo na kinyesi kutoka kwenye ndege zinazowasili kutokea China. Maji hayo machafu yanaweza kuchambuliwa kitaalamu na kugundua kwa wastani ni abiria wangapi wana maambukizo ya UVIKO-19, na pia aina za virusi walivyonavyo. 

Miongoni mwa mataifa ambayo tayari yameshatangaza nia ya kufanya vipimo hivyo ni Ubelgiji, Kanada, Austria na Australia. Umoja wa Ulaya unatazamiwa  pia kufanya hivyo baada ya maafisa wake wengi kupendekeza hatua hiyo. Na, kwa mujibu wa vyombo vya habari, Marekani nayo iko mbioni kuchukua hatua hiyo.

Soma pia: China yakosoa vizuizi vya UVIKO dhidi ya raia wake

Maambukizo yanaripotiwa kuzidi nchini China tangu mwezi uliopita wakati taifa hilo la Asia lilipoanza kusitisha hatua zake za udhibiti wa maambukizo zilizokuwapo tangu janga lianze mwishoni mwa mwaka 2019.

Mfanyakazi wa afya mjini Rome akingojea wasafiri kutoka China katika uwanja wa ndege wa Leonardo da Vinci siku ya Alhamis (Disemba 29).Picha: Alessandra Tarantino/AP Photo/picture alliance

Nchi nyingi, ikiwemo Marekani, zinawataka abiria wanaowasili kutoka China wawe na vyeti vinavyoonesha hawana maambukizo ya UVIKO-19, hatua ambayo imeikera sana Beijing.

Utafiti kujuwa kiwango halisi cha maambukizo

Mkurugenzi wa Taasisi ya Afya Duniani yenye makao yake Geneva, Uswisi, Antonie Flahault, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba "hata kama upimaji maji machafu hauwazuwii watu wenye maambukizo, angalau unatoa taswira ya kinachoendelea sasa nchini China."

Siku ya Jumatano, Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO, lilikosoa kile lilichokiita "fasili finyu" ya vifo vinavyotokana na UVIKO-19 inayotolewa na China na kusema kuwa maafisa wa nchi hiyo wanaripoti idadi ndogo zaidi kuliko wagonjwa wanaolazwa na kufa kwa maradhi hayo.

Soma pia: Maambukizo ya UVIKO-19 yarudi upya China

Kwa mujibu wa Flahault, kuyapima maji machafu kutasaidia kujaza matomotomo yaliyoonekana kwenye ripoti za China juu ya kiwango cha maambukizo. "Kujuwa kwamba kiasi cha asilimia 30 mpaka 50 cha abiria kutoka China wameambukizwa ni jambo muhimu katika wakati ambapo hakuna takwimu za kuaminika." Alisema.

Upimaji huo pia utaziruhusu nchi kugunduwa aina mbalimbali mpya za virusi ambazo zinaweza kubadilisha kabisa muelekeo wa maradhi yenyewe, kama ilivyotokea kwa aina ya Omicron mwaka 2021.

Hofu ya kuzuka kwa aina mpya ya virusi

Wasafiri kutoka China huenda wakazuiwa kuingia nchi za Ulaya ikiwa hawana vyeti vya kupima UVIKO-19.Picha: Andy Wong/AP/dpa/picture alliance

Wataalamu wanahofia kwamba mripuko wa maambukizo mapya ya UVIKO-19 katika taifa lenye watu bilioni 1.4 unaweza kuwa mazalio makubwa ya aina mpya za virusi vya korona.

Upimaji wa maji machafu ni jambo rahisi na jepesi zaidi kuliko kuwapima abiria wanaowasili kwenye viwanja vya ndege.

Tawi la Baraza la Viwanja vya Ndege vya Kimataifa barani Ulaya, ambalo limepuuzilia mbali uwezekano wa kuwapima abiria wanaowasili kutoka China, linapigania kuwepo kwa upimaji wa maji machafu.

Ongezeko la maambukizi ya COVID-19 Ujerumani

02:57

This browser does not support the video element.

Lakini mtaalamu wa virusi nchini Ufaransa, Vincent Marechal, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hata njia hii haimaanishi kutoa jawabu kamili na la moja kwa moja kuhusu kiwango cha maambukizo kwa abiria waliokuwamo kwenye ndege, kwa sababu kinaweza tu kuwapima wale waliotumia choo wakiwamo humo.

Vile vile, inachukuwa muda mrefu kukusanya, kupima, kupanga na kuchambua ugunduzi ambao, nao hatimaye, hauwezi kuhusishwa na abiria fulani makhsusi.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW