Madaktari bingwa wa ubongo wakutana Tanzania
16 Aprili 2026
Akizindua mkutano huo, Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya afya, hususan katika huduma za kibingwa za upasuaji wa ubongo na mfumo wa fahamu. Ameeleza kuwa juhudi hizo zimewezesha ongezeko la madaktari bingwa kutoka 138 mwaka 2020 hadi 145 mwaka 2025, ambapo saba kati yao ni wanawake, hatua inayodhihirisha dhamira ya kuimarisha rasilimali watu katika sekta hiyo nyeti.
"Katika miaka ya hivi karibuni, tumewekeza katika matibabu ya upasuaji wa ubongo na mfumo wa fahamu pamoja na rasilimali watu, ambapo idadi ya madaktari bingwa imeongezeka kutoka 138 mwaka 2020 hadi 145 mwaka 2025, kati yao saba ni wanawake.”
Katika mjadala wa mkutano huo, imeelezwa kuwa Afrika inakabiliwa na changamoto kubwa ya majeraha ya ubongo yanayosababishwa na ajali za barabarani. Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amesema ongezeko la ajali hizo linachangiwa kwa kiasi kikubwa na ukuaji wa kasi wa usajili wa magari pamoja na changamoto za miundombinu na usalama barabarani.
Takwimu zilizowasilishwa zinaonesha kuwa bara la Afrika lina wastani wa vifo 26.6 kwa kila watu 100,000 vinavyotokana na ajali za barabarani,kiwango ambacho ni cha juu zaidi ikilinganishwa na wastani wa dunia wa vifo 15 kwa kila watu 100,000.
"Hali hii inaonyesha ongezeko la kutisha la hivi karibuni, linalochangiwa kwa kiasi kikubwa na ongezeko la kasi la usajili wa magari barani humo.”
Kwa mtazamo wa kimataifa, viongozi wa sekta hiyo wameonya kuhusu pengo kubwa la upatikanaji wa huduma za upasuaji wa ubongo duniani.
Kuna pengo kubwa la upatikanaji huduma za upasuaji wa ubongo duniani
Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Shirikisho la Dunia la Vyama vya Upasuaji wa Ubongo na Mfumo wa Fahamu, Tarick Khan, amesema zaidi ya watu bilioni tano duniani hawana upatikanaji wa huduma salama na za wakati mwafaka za upasuaji wa ubongo, hali inayohitaji hatua za haraka za kimataifa ili kuhakikisha usawa katika huduma za afya.
"Tupo hapa kujadili usawa, upatikanaji wa huduma, na thamani tunayoweka kwenye maisha ya binadamu.”
Aidha, mkutano huo umeweka historia kwa kuzinduliwa rasmi kwa Shirika la Kimataifa la Upasuaji wa Ubongo na Mfumo wa Fahamu (ISGN), jukwaa jipya la ushirikiano wa kimataifa linalolenga kuimarisha upatikanaji wa huduma hizo, kukuza mafunzo ya wataalamu na kuboresha uwekezaji katika vifaa tiba.
Hatua hii inatarajiwa kuleta mchango mkubwa katika kuimarisha huduma za upasuaji wa ubongo si tu nchini Tanzania bali pia katika ukanda wa Afrika Mashariki na bara la Afrika kwa ujumla.
Kwa ujumla, wadau wamekubaliana kuwa kuna haja ya kuchukua hatua za pamoja katika kupunguza ajali za barabarani, kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili kukabiliana na ongezeko la majeraha ya ubongo na mishipa ya fahamu, ambalo linaendelea kuwa changamoto kubwa ya afya ya umma barani Afrika.