1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiSomalia

Wataalamu wa hali ya hewa watahadharisha juu ya El Nino

9 Juni 2023

Wanasayansi wa Marekani wamesema mfumo wa hali ya hewa unaojulikana kama El Nino umeanza katika bahari ya Pasifiki na kuongeza wasiwasi wa ongezeko la joto duniani.

ECUADOR-WEATHER-FLOODS
Watu wakipita juu ya barabara zilizofunikwa na mafuriko nchini Ecuador.Picha: AFP via Getty Images

Hali hiyo imesababisha baadhi ya mataifa kujiandaa mapema na hali mbaya ya hewa ikiwemo vimbunga na mafuriko hasa katika mataifa ya Amerika ya Kusini na Pembe ya Afrika.

Mamlaka ya hali ya hewa ya Marekani NOAA imetahadharisha kuwa El Nino huenda ukaufanya mwaka ujao 2024 kuwa mwaka wenye joto zaidi duniani.

Soma pia:Idadi ya waliokufa kwa mafuriko Rwanda yafikia 130

Tofauti na mfumo wa hali ya hewa wa La Nina, ambao aghalabu hupunguza viwango vya joto duniani na ambao umeshuhudiwa kwa miaka mitatu iliyopita, kinyume chake El Nino inahusishwa na kupanda kwa viwango vya joto.

Wataalamu hao wa hali ya hewa wanahofia kuwa joto huenda likapindukia kiwango cha nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Celcius.

Tom Di Liberto ambaye mwanasayansi kutoka mamlaka ya hali ya hewa ya Marekani NOAA amesema, "Mwaka 2024, nadhani ni mwaka ambao utakuwa na joto litakalovunja rekodi, na kutokana na ongezeko la joto duniani tangu mwaka 2016, El Nino huenda ikachangia viwango hivyo kupanda hata zaidi. Lakini lolote linaweza kutokea kwa sababu hali ya hewa inabadilika badilika."

Maeneo gani yataathirika na El Nino?

Moja kati ya athari ya El Nino ni kuongeza viwango vya joto na ukamePicha: Rungroj Yongrit/dpa/picture alliance

El Nino inatajwa pia huenda ikaathiri mfumo wa hali ya hewa duniani, hasa kuchochea hali ya ukame nchini Australia, mvua kubwa kusini mwa Marekani na joto kupanda katika viwango vya kutisha nchini Japan na sehemu nyengine duniani. Eneo la pembe ya Afrika linatarajiwa kupata mvua na kuongeza matumaini ya angalau kupunguza makali ya ukame.

Mfumo huo wa hali ya hewa ulitokea mara ya mwisho mnamo mwaka 2018-19 na hushuhudiwa kwa wastani kila baada ya miaka miwili hadi saba.

Wanasayansi wametadharisha kuwa hali huenda ikawa mbaya zaidi mwaka huu. Mara ya mwisho kwa ulimwengu kushuhudia El Nino ilikuwa mwaka 2016 ambapo kulikuwepo na joto kali.

Wanasayansi hao wanatabiri kuwa El Nino ya mwaka huu, ukijumuisha pia na athari za mabadiliko ya tabia nchi, kutaufanya ulimwengu kuwa na joto zaidi.

Soma pia: UN: Zaidi ya Wasomali 140,000 wakimbia makwako kutokana na msimu wa mvua za mafuriko

Kando na kupanda kwa viwango vya joto, athari nyengine ni hasara ya kiuchumi. Kulingana na utafiti uliochapishwa mwezi uliopita katika jarida la Sayansi, wataalamu wameeleza kuwa, ulimwengu huenda ukapata hasara ya hadi dola trilioni 3 za Marekani.

Hali mbaya ya hewa inatajwa kuwa na mahusiano ya moja kwa moja na kupungua kwa uzalishaji wa kilimo, viwanda na kuchangia kuenea kwa magonjwa.

Serikali katika nchi ambazo zinatajwa kuwa hatarini tayari zimeanza kuweka mikakati ya kukabiliana na athari hasi ya El Nino. Kwa mfano, Peru imetenga dola bilioni 1.06 huku Ufilipino ikiunda timu maalum ya kushughulikia athari zozote ambazo zinaweza kujitokeza wakati wa El Nino.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW