1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria na Urusi zashutumiwa kukwamisha shughuli za OPCW

16 Aprili 2018

Mwanadiplomasia wa Uingereza amesema Urusi na Syria wamewazuwiya wachunguzi wa shirika la kudhibiti silaha za sumu OCPW kuingia mjini Douma kuchunguza madai ya shambulizi la silaha za kemikali mjini humo.

Niederlande OPCW-Sondersitzung zu mutmaßlichem Giftgaseinsatz in Duma
Picha: Getty Images/AFP/K. van Weel

Kulingana na balozi wa Uingereza nchini Uholanzi Peter Wilson, mkuu wa shirika la OCPW Ahmet Uzumcu, ameuambia mkutano wa hadhara kwamba wachunguzi wake wameshindWa kupata nafasi au ruhusa ya kuingia mjini Douma.

Wilson amesema Serikali ya Syria pamoja na Urusi wamewanyima nafasi wachunguzi hao kuingia mjini humo kwa sababu za kiusalama, amesema mpaka sasa bado hawajaweza kuhakikishiwa usalama wao na haijawa wazi ni lini hasaa hilo litakapofanyika.

Picha: picture alliance/AP Photo/M. Kooren

Kundi hilo lilitarajiwa kuanza kazi hapo jana baada ya kuwasili mjini Damascus siku ya Jumamosi. Lakini badala yake walikutana na maafisa katika hoteli moja mjini humo na hakukuwepo na chombo chochote cha habari kilichokubaliwa kufuatilia mkutano huo. Hata hivyo Urusi na Syria wamekanusha madai ya kuwazuwiya wachunguzi hao kuingia mjini douma.

Aidha wataalamu wanadai kemikali ya Chlorine pamoja na Sarin zilitumika katika shambulizi hilo la douma mnamo Aprili 7 na kusababisha mauaji ya watu 40.

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya watoa wito wa suluhu la kisiasa Syria

Huku hayo yakiarifiwa Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya wamesema wanaunga mkono juhudi zote zinazoweza kuizuwiya Syria kutumia silaha za sumu na kutoa wito wa kupatikana suluhu la kisiasa kwa mgogoro wa Syria uliyodumu miaka 7 sasa. Mwaziri hao 28 wamekosoa shambulizi la kijeshi linalioungwa mkono na Urusi kwamba serikali ya Syria inapigana dhidi ya waasi na kuitisha usitishwaji wa mapigano haraka ili kutoa nafasi ya upatikanaji wa misaada ya kiutu.

Picha: Getty Images/AFP/E. Dunand

Katika taarifa ya pamoja baada ya mazungumzo mjini Luxembourg mawaziri hao wa Umoja wa Ulaya wamemlaumu rais Bashar al Assad kwa shambulizi la mjini Douma na kuunga mkono mashambulizi yaliyofanywa siku ya Jumamosi na Marekani Ufaransa na Uingereza siku ya Jumamosi linasemekana kuharibu hifadhi ya kemikali za sumu nchini Syria. 

Kwa upande wake Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema Umoja wa Ulaya umeungana katika wakati muhimu wa kutaka kulinda na kuondoa kabisa matumizi ya sialaha za kemikali.  Naye Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema shambulizi la majibu kutoka nchi za Magharibi lililofanyika siku ya jumamosi lilihitajika lakini wanachama wengine wa Umoja huo wamekuwa makini  kuzungumzia hilo ili kuepusha mgogoro uliyopo kupanuka zaidi.

Mwandhishi: Amina Abubakar /AFP/dpa/rEUTERS 

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW