1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waitia hatiani Rwanda kushirikiana na M23

5 Agosti 2022

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema wana ushahidi wa kutosha kwamba vikosi vya jeshi la Rwanda vinafanya operesheni katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo kuliunga mkono kundi la waasi wa M23.

Archivbild I M23-Rebellen
Picha: Jerome Delay/AP/picture alliance

Katika ripoti mpya kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wataalamu hao wamevilaumu vikosi vya Rwanda kwa kukiuka vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo kwa muingilio wa moja kwa moja katika taifa hilo aidha kuliunga mkono kundi la waasi la M23 ama kufanya operesheni za kijeshi dhidi ya kundi lingine la waasi la Democratic Forces for Liberation of Rwanda, FDLR. Haya yameripotiwa na shirika la habari la AP.

Kundi hilo la wataalamu limeongeza kuwa wanajeshi wa Rwanda pia walikiuka vikwazo kwa kutoa silaha, risasi na sare kwa waasi wa M23.

Hali ya usalama inatia wasiwasi

Ripoti hiyo imesema licha ya takriban miezi 15 ya hali inayoendelea ya kuzingirwa katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na operesheni za kijeshi zinazofanywa na majeshi ya nchi hiyo, vikosi vya Uganda, na wanajeshi kutoka kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa MONUSCO, hali ya usalama na kibinadamu katika maeneo hayo mawili  imebaki kuwa ya kutia wasiwasi mkubwa.

Wataalamu hao pia walitaja hali inayozidi kuzorota katika maeneo ya Rutshuru na Nyiragongo Kaskazini mwa Kivu.

Wakaazi wa mashariki mwa Kongo wakikimbia mashambulizi ya makundi ya waasiPicha: Dai Kurokawa/dpa/picture alliance

Wataalamu hao wameongeza kuwa mashambulizi kutoka kwa wapiganaji wa M23 yamekuwa ya mara kwa mara, marefu na thabiti na eneo wanalolithibiti limeongezeka pakubwa na kusababisha idadi kubwa ya watu kupoteza makazi yao huku pia kukiwa na mashambulizi ya kiholela.

Ripoti hiyo imesema kuwa waasi hao wa M23 wanawauwa raia kwa maksudi na kutumia mbinu ya kuvishambulia vikosi vya MONUSCO.

Vikosi vya Kongo pia vyadaiwa kujiunga na makundi yanayojihami

Wataalamu hao wanasema baadhi ya vikosi vya Jamhuri ya Kideomkrasi ya Kongo viliingia katika ushirikiano wa muda na makundi ya kujihami katika eneo hilo kupigana na waasi wa M23 yakiwa peke yao ama kwa ushirikiano na vikosi vingine vya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Ripoti hiyo imeendelea kusema kuwa makundi hayo yaliojihami yalipewa silaha, risasi na sare na baadhi ya wanajeshi wa nchi hiyo.

Wataalamu hao wameongeza kuwa msaada kwa makundi kadhaa ya kujihami katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na ushirikiano nayo kutoka kwa vikosi vya serikali huko Rutshuru pia ilikiuka vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa.

Kundi hilo la wataalmu limesema ukiukwaji wa haki za binadamu za kimataifa na sheria za kibinadamu,

ikiwa ni pamoja na mauaji ya makusudi ya watoto na raia na pamoja na mashambulizi ya makombora yakiholela  yaliyosababisha vifo vya raia na kuharibu nyumba na shule, vilivyofanywa zaidi na kundi la waasi la M23, pia ni vitendo vinavyoweza kusababisha vikwazo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW