UN wasema makundi ya kigaidi yana uhuru Afghanistan
8 Februari 2022Katika ripoti hiyo iliyosambazwa Jumatatu, wataalaamu hao wamesema makundi yenye msimamo mkali, yanayohusishwa na mtandao wa Al-Qaida na kundi linalojiita Dola la Kiislam, IS, yamefanikiwa kujipenyeza barani Afrika, hasa katika ukanda wa Sahel wenye misukosuko.
Wamesema wapiganaji wa Dola la Kiislamu wameendelea kufanya kazi kama kundi la uasi wa chini kwa chini uliojiimarisha katika mataifa ya Iraq na Syria, ambako waliwahi kujitangazia utawala wake waliouita ukhalifa baada ya kudhibiti maeneo makubwa ya mataifa hayo mawili kuanzia 2014 hadi 2017, wakati waliposhindwa na majeshi ya Iraq kwa msaada wa muungano unaoongozwa na Marekani.
Soma pia:Taliban wamkamata mpiganaji aliemuuwa mwanamke wa Hazara
Ripoti hiyo iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na jopo la wataalamu linalofuatilia vikwazo dhidi ya Al-Qaida na Dola la Kiislamu, IS, imesema kurejea kwa Taliban madarakani Agosti 15 katikati mwa machafuko yaliyosababishwa na harakati za mwisho za kuondoka kwa wanajeshi wa Meriekani na NATO baada ya miaka 20 ya kukaliwa nchi hiyo, lilikuwa ni tukio la muhimu zaidi la miezi sita ya mwisho ya 2021.
Kundi la Taliban liliitawala Afghanistan kwa mara ya kwanza kuanzia 1996-2001 na kuondolewa madarakani kwa madai ya kulihifadhi kundi la Al-Qaida na kiongozi wake, Osama bin Laden, aliyedaiwa kuongoza mashambulizi ya kigaidi ya Septemba11, 2001 nchini Marekani.
Ahadi ya kupambana dhidi ya ugaidi
Katika makubaliono ya Februari 2020 yaliyoainisha masharti ya kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistani, kundi la Taliban liliahidi kupambana dhidi ya ugaidi na kuyanyima makundi ya kigaidi, mahala salama nchini Afghanistan.
Lakini kamati ya wataalamu imesema hakuna ishara zozote za karibuni kwamba Taliban wamechukwa hatua kupunguza shughuli za wapiganaji wa kigeni nchi humo.
Kinyume chake, wamesema wataalamu hao kuwa makundi ya kigaidi yanafurahia uhuru zaidi, ingawa mataifa wanachama hawajaripoti uhamishaji wowote mpya mkubwa wa wapiganaji wa kigeni kuingia nchini Afghanistan.
Wataalamu wamebaini kuwa Al-Qaida ilitoa taarifa ya kuwapongeza Taliban kwa shindi wao wa Agosti 31, lakini tangu wakati huo kundi hilo limeendeleza ukimya wa kimkakati ambao yamkini unalenga kuepusha kuhatarisha juhudi za Taliban kupata utambuzi na uhalali wa kimataifa.
Soma pia: Utawala wa Taliban wasema uko karibu kutambuliwa kimataifa
Al-Qaida inaendelea kujiimarasha baada ya mkururo wa vifo vya viongozi wake na inaelezwa kukosa uwezo kwa sasa wa kufanya mashambulizi makubwa ya nje, jambo amabalo linasalia kama lengo lake la muda mrefu kwa mujibu wa watalamu hao.
Kiongozi wa Al-Qaida, Ayman al-Zawahri aliripotiwa kuwa hai mwezi Januari 2021, lakini mataifa ya Magharibi yanaendelea kuamini kwamba kiongozi huyo ana hali mbaya kiafya.
Hofu ya makundi ya kigaidi Afrika
Kwa upande wa kundi la Dola la Kiislamu, wataalamu wamesema ingawa linadhibiti maeneo machache nchini Afghanistan, limeeonesha uwezo wa kuendeleza mashambulizi makali na hivyo kuzidisha hali tete ya kiusalama nchini humo.
Wametolea mfano wa shambulio la Agosti 27 dhidi ya uwanja wa ndege wa Kabul ambapo zaidi ya watu 180 waliuawa.
Soma pia: Taliban na Magharibi waijadili hali nchini Afghanistan
Baadhi ya mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa yamesema nguvu ya Dola la Kiislamu imepanda kutoka wapiganaji karibu 2,200 na kufikia takribani 4,000 kufuatia kuachiwa kwa maelfu ya wafungwa ambao inakadiriwa kuwa nusu yao walikuwa wapiganaji wa kigeni.
Wataalamu wamesema, mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa pia yana wasiwasi juu ya mafanikio ya matawi ya IS na Al-Qaida barani Afriaka katika nusu ya mwisho ya mwaka 2021.
Chanzo: AP