Wataalamu wa UN: Mahasimu Sudan wanatumia njaa kama silaha
27 Juni 2024Hayo ni wakati kukiwa na onyo linaloongezeka kuhusu kuzuka kwa baa la njaa nchini humo. Wataalamu hao wamesema vikosi vya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF vinatumia chakula kama silaha na kuwaacha raia wateseke kwa njaa. Wanasema kiwango cha njaa na watu kupoteza makaazi yao kinachoonekana nchini Sudan hakijawahi kushuhudiwa kabla.
Soma pia: Ulaya yawawekea vikwazo maafisa 6 wa kijeshi wa Sudan
Mapigano yaliyodumu kwa miezi 14 yamewauwa zaidi ya watu 14,000 na kuwajeruhi wengine 33,000, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, lakini wanaharakati wa haki wanasema idadi hiyo huenda ikawa juu zaidi.
Zaidi ya watu milioni 11 wamelazimika kuyakimbia makaazi yao. Watalaamu wa Umoja wa Mataifa wanaonya kuwa baa la njaa linakaribia nchini humo kwa sababu msaada wa kiutu umezuiwa na msimu wa mavuno ulitatizwa kwa sababu ya vita. Wameongeza kuwa zaidi ya raia milioni 25 nchini Sudan na wale walioikimbia nchi wanateswa kwa kunyimwa chakula na wanahitaji msaada wa dharura wa kibinaadamu.