Wataalamu wa usafirishaji waangazia changamoto za Afrika
21 Agosti 2025
Msongamano wa magari, na ubovu wa miundombinu ya barabara vinatajwa kuwa changamoto zinazoyakabilia mataifa mengi duniani hasa bara la Afrika.
Hayo yameelezwa leo na watafiti na wataalamu wa usafiri na usafirishaji wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Usafirishaji, jijini Dar es Salaam na kueleza namna ya kukabiliana na changamoto hizo.
Akizungumza katika mkutano huo, Mhandisi Ephata Mlay kutoka Wakala wa Barabara Tanzania, TANROADS, amesema Tanzania inakabiliwa na tatizo kubwa la msongamano wa magari na hivyo ili kukabiliana nalo, taifa hilo linatekeleza Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi, BRT.
''Msongamano wa magari ni mkubwa Tanzania na ili kukabiliana tunataka kuhamasisha matumizi ya usafiri wa umma, ambao ni haya mabasi yaendayo kasi" alisema Mlay.
Wataalamu wazungumzia matumizi ya taka za plastiki
Profesa Guojing Jing, wa Chuo Kikuu cha Jiotong, Japan, alizungumza katika mkutano huo na kueleza namna nchi za Afrika zinavyoweza kutumia taka za plastiki kutengeneza Barabara bora na zenye kudumu.
''Hapa Tanzania naona kuna maeneo mengi yenye taka za plastiki ambazo zinaweza kurejelezwa, na kutumika vyema katika ujenzi wa miundombinu. Taka za plastiki zikitumika kwenye ujenzi wa barabara au reli zina uwezo wa kuzifanya barabara zidumu kwa zaidi ya miaka 40. Tanzania inaweza kufanya hivi pia, watafiti wanaweza kulichukua hili.''
Awali akifungua mkutano huo, Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Makame Mbarawa amesema sekta ya usafirishaji ndio uti wa mgongo wa uchumi wa taifa lolote duniani, hivyo tafiti zinazofanyika kuhusu sekta hiyo zitumike ili zisaidie kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya usafiri.
Mkutano wa siku mbili, ulioanza Agosti 21 na unaotarajiwa kumalizika Agosti 22, umewakutanisha wadau wa usafiri na usafirishaji na watafiti kutoka Ujerumani, China, Marekani, Uingereza, Norway, Nigeria, Burkina Faso na Kenya.