1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataalamu wa WHO kukutana kuijadili chanjo ya AstraZeneca

Zainab Aziz Mhariri:Yusuf Saumu
16 Machi 2021

Wataalam wa shirika la afya ulimwenguni WHO wajiandaa kukutana Jumanne kujadili juu ya chanjo ya AstraZeneca ambayo nchi kadhaa pamoja na za Ulaya zimesimamisha kutolewa kwake.

Weltspiegel 15.03.2021 | Corona | AstraZeneca-Impfstoff
Picha: Dado Ruvic/REUTERS

Mgogoro wa AstraZeneca umejitokeza wakati ambapo nchi kadhaa duniani zinapambana na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona. Mataifa matatu makubwa ya Ulaya, Ujerumani, Italia na Ufaransa yamejiunga na mengine kusimamisha chanjo hiyo ya AtraZeneca hilo likiwa ni pigo kwa kampeni ya utoaji chanjo ulimwenguni dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 ambao umesabaisha vifo vya zaidi ya watu milioni 2.6.

Waziri Spahn amewataka wale ambao tayari wamepokea chanjo hiyo ya AstraZeneca na katika zaidi ya siku nne baada ya kupokea chanjo hiyo wanajisikia vibaya, kwa mfano wana maumivu ya kichwa au ngozi zao kuwa na malengelenge wapate matibabu ya haraka.

Waziri wa afya wa Ujerumani Jens SpahnPicha: Annegret Hilse/REUTERS

Mtaalam kwenye Taasisi ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza nchini Ujerumani ya Robert Koch,  Dirk Brockmann amesema nchini Ujerumani idadi ya watu walioambukizwa iliongezeka kwa asilimia 20 hadi wiki iliyomalizika, wakati taifa hilo likiwa limeanza kulegeza hatua za karantini polepole. Amesema hatua hiyo si muafaka kwa sasa kwani kutokana na kuongezeka kasi ya aina mpya ya virusi aina ya B117 kutokea Uingereza kulegeza taratibu za karantini sio sawa.

Taasisi ya Robert Koch imeorodhesha maambukizi mapya 5,480 katika muda wa saa 24 zilizopita. Sasa  jumla ya watu 2,581,329 wameambukizwa nchini Ujerumani. Idadi ya vifo pia imeongezeka kwa watu 238 zaidi na kufikisha idadi ya watu 73,656 waliokufa hadi sasa. Madaktari wanaowahudumia wagonjwa mahututi nchini Ujerumani wameshauri kurudishwa mara moja hatua za karantini kwa ajili ya kuzuia kuenea wimbi la tatu la virusi vya corona.

Rais wa Brazil Jair BolsonaroPicha: Sergio Lima/AFP/Getty Images

Kwingineko maambukizi ya COVID-19 na vifo vimeongezeka nchini Brazil. Rais Jair Bolsonaro amethibitisha kwamba atateua mtaalam wa magonjwa ya moyo Marcelo Queiroga kuwa waziri wa afya huku akimtumbua waziri wa afya wa sasa Eduardo Pazuello. Marcelo Queiroga atakuwa waziri wa afya wa nne nchini Brazil katika kipindi cha mwaka mmoja.

Nchini Urusi watengenezaji wa chanjo ya Sputnik V iliyopata mafanikio wamesema wamefikia makubaliano kuhusiana na chanjo hiyo na nchi muhimu za Ulaya. China pia imetengeneza chanjo za Covid-19 na imeanza kuzisafirisha ulimwenguni kote ikiwa ni pamoja na katika nchi za barani Ulaya, Mashariki ya Kati na Amerika ya Kusini.

Vyanzo:/AFP/https://p.dw.com/p/3qfuf

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW