Wataalamu wamshauri Bi Clinton kutaka kura zihesabiwe upya
24 Novemba 2016Kundi la wataalamu hao limetoa ushauri huo wakati mshindi wa uchaguzi huo Donald Trump akiendelea na mchakato wa kuwateuwa maafisa watakaoshika nyadhifa muhimu katika utawala wake.
Kulingana na ripoti iliyochapishwa katika toleo la Jumanne la jarida la New York Magazine, wataalamu hao ambao ni pamoja na mwanasheria maarufu kuhusu haki ya kupiga kura John Bonifaz, na mkuu wa kitengo cha usalama wa kompyuta katika chuo kikuu cha Michigan J. Alex Halderman, wamesema kuna uwezekano kwamba Bi Hillary Clinton alipewa kura chache kuliko alizopigiwa katika majimbo kadhaa ya uchaguzi yanayotegemea mfumo wa kielektriniki kukusanya na kutoa matokeo.
Miongoni mwa majimbo yanayoshukiwa kuathiriwa na hali hiyo, ni yale muhimu katika kuamua mshindi wa rais, kama vile Wisconsin, Michigan na Pennysylvania.
Hakuna ushahidi wa kutokea hitilafu
Hata hivyo, katika makala aliyoiandika katika jarida la New York Magazine John Bonifaz amesema kundi lake halina ushahidi wa kutokea mashambulizi ya kimtandao, wala hitilafu katika upigaji kura, na kuongeza kuwa ni vyema kura zihesabiwe upya ili kuondoa mashaka. Donald Trump aliyashinda kwa idadi ndogo kabisa majimbo hayo matatu, ambayo miaka ya hivi karibuni yamekuwa yakichukuliwa na chama cha Democratic.
Kambi ya Bi Clinton, ilijizuia kutangaza chochote kuhusu hali hii mpya ilipoulizwa kutoa maoni, na wala haikusema chochote juu ya iwapo itataka kura zihesabiwe upya katika majimbo hayo. Hali kadhalika kambi ya Donald Trump imesalia kimya kuhusu suala hilo.
Mchakato wa kuhesabu kura, karatasi baada ya karatasi, na kuhakiki vifaa vya upigaji kura unachukua muda mrefu na ni wa gharama kubwa, na unaweza kuanzishwa tu ikiwa kampeni ya Hillary Clinton itaomba kufanya hivyo.
‘Njia pekee ya kuwa na uhakika kuwa mashambulizi ya kimtandao hayakupotosha matokeo ya kura ni kuvifanyia uhakiki vithibitisho vilivyopo‘‘ Ameandiaka Halderman katika makala yake. Jimbo la Pennsylvania lakini limesema litachukua hatua binafsi ya kuhakisha kura zake.
Makovu yaweza kutoneshwa
Mwito huu wa kuhesabiwa upya kwa kura katika majimbo hayo baada ya kampeni iliyokuwa na mivutano mikubwa bila shaka utapokelewa kwa furaha na wademocrat, na kupingwa vikali na warepublican, ambao mgombea wao Donald Trump alipata ushindi kupitia mfumo wa kujumlisha kura maalum za majimbo. Kwa upande wa kura moja moja iliyopigwa, matokeo ya hivi sasa yanaonyesha Hillary Clinton akimzidi Trump kwa kura milioni 2.
Tayari Trump ambaye ni Rais Mteule anaendelea na mchakato wa kuwateuwa maafisa wataoshikilia nyadhifa muhimu katika utawala wake.
Katika kile kilichochukuliwa na wachambuzi kama ishara ya kulegeza msimamo dhidi ya wahamiaji na makundi ya wachache, amemteuwa Nikki Haley kuwa balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, wadhifa ambao ni ya hadhi ya uwaziri.
Nikki Haley, mwanamke ambaye wazazi wake ni wahamiaji kutoka India, hivi sasa ni gavana wa jimbo la South Carolina, akiwa mwanamke wa kwanza, na mtu ambaye si mzungu, kushika wadhifa huo.
Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, afpe
Mhariri:Caro Robi