Wataalamu wataka gharama za huduma za intaneti kupunguzwa
15 Februari 2024Mkutano Mkuu wa Kimataifa unaowakutanisha washirika wa kimkakati wa teknolojia, maarufu kama "Future Ready Summit," umefanyika Alhamisi jijini Dar es Salaam huku wadau wa sekta hiyo wakitilia mkazo masuala manne - kupunguzwa gharama za intaneti, kupunguzwa bei za vifaa vya teknolojia, matumizi jumuishi ya intaneti kwa makundi yote, wakiwamo wanawake, sera na sheria rafiki za matumizi ya dijitali.
Wadau katika mkutano huo walielezwa kuwa ipo haja ya kuimarisha miundombinu ya intaneti Tanzania, kwani takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya watu bilioni 2 duniani waishio vijijini bado wanakabiliwa changamoto ya upatikanaji wa intaneti.
Soma pia:Miaka 20 ya Smartphone Barani Afrika
Washiriki katika mkutano huo uliondaliwa na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom, wametakiwa kuweka mikakati ya pamoja ili kuimarisha miundombinu ya teknolojia ya habari na mawasiliano, ujumuishi wa dijitali na fedha na kuwahamasisha watu kuchangamkia fursa za kidijitali.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Kassim amewataka wadau kufanya tathmini ni kwa namna gani wanawake watashiriki katika uchumi wa kidiitali.
"Makampuni ya simu, wekeni gharama nafuu za intaneti ili kuhimiza wananwake kushiriki katika uchumi wa kidjitali. Tunatamani kuona kila mtanzania anapata intaneti mpaka vijijini," alisema Majaliwa, akiwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo w akila mwaka.
Waziri Mkuu Majaliwa aliitaka wizara husika ibebe changamoto za kisera na sheria zilizoainishwa na wadau ili kutengeneza mazingira rafiki ya matumizi ya kidijitali.
Tofauti ya matumizi kati ya wanaume na wanawake
Mkuu wa kitengo cha Mamlaka ya Masoko na Mazingira wa Umoja wa Mawasiliano (ITU), Sofie Maddens, pia alisisitiza suala la ushiriki wa wanawake katika matumizi ya dijitali.
Maddens alisema bado kuna ombwe kati ya wanawake na wanaume kwenye matumizi ya intaneti na vifaa vya teknolojia kwani asilimia 70 ya wanaume duniani wanatumia intaneti huku asilimia 65 tu ya wanawake ndio wanaotumia intaneti.
"Ikiwa wanawake watakosa mtandao, ikiwa hawawezi kumudu gharama za kununua vifaa, au kujisikia salama wanapokuwa mtandaoni, tunawezaje kuwatarajia kufanya uvumbuzi ujao wa kuibadili dunia, au kushiriki katika uvumbuzi wa kidigitali."
Soma pia: TEKNOHAMA kuinua kilimo Afrika
Maddens amesisitiza kuwa ujio wa akili ya kubuni (AI) ni sehemu ya Maendeleo yaTeknolojia na tunatakiwa kushirikiana kuifahamu.
Mkurugenzi wa Vodacom, Phillipi Bassiimire alizungumzia nia ya kampuni hiyo kushusha gharama za vifaa vya digitali ili kupambana na mgawanyo wa kidigitali. Amehimiza ushirikiano wa wadau mbalimbali ili kupambana na suala hilo.
Mkutano huu umewakutanisha wadau wa teknolojia na washirika wa kimkakati ili kujadili kwa pamoja masuala yanayochochea maendeleo ya teknolojia Afrika.