Wataalamu wataka vikosi vya Mali na Wagner vichunguzwe
1 Februari 2023Wataalamu huru wa haki za binaadamu wametoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu uwezekano wa unyanyasaji, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu unaofanywa na vikosi vya serikali ya Mali na wapiganaji wa kampuni binafsi ya kijeshi ya Urusi ya Wagner Group.
Wataalamu hao wanaofanya kazi na Umoja wa Mataifa wamesema wamepokea taarifa kuhusu mauaji ya kutisha, makaburi ya watu wengi, ubakaji, unyanyasaji wa kijinsia na uhalifu mwingine unaodaiwa kufanywa katika kipindi cha miaka miwili kwenye mji wa Mopti na maeneo mengine ya Mali.
Soma zaidi: Umoja wa Mataifa wataka kuchunguza mauwaji ya Mali
Wamesema wana wasiwasi kwamba shughuli za kijeshi zinakabidhiwa kwa kikosi mamluki cha Wagner, jambo linalochochea vurugu.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, kuna hali ya ugaidi na kulipiza kisasi dhidi ya watu wanaojaribu kuzungumza na tayari wamewasilisha taarifa hizo kwa serikali ya mjini Bamako.