Wataliani wapiga kura
4 Machi 2018Mashirika yanayofanya utafiti wa maoni ya wapiga kura yanatabiri kwamba waziri mkuu wa zamani Silvio Berlusconi na washirika wake wa siasa kali za mrengo wa kulia wataibuka kuwa kundi kubwa bungeni, lakini wakikosa wingi wa kutosha.
Vuguvugu la kupinga utawala la 5-Star linaonekana litakuwa chama kikubwa pekee, kikipata nguvu kutokana na wapiga kura kutoridhishwa na rushwa iliyoota mizizi na ongezeko la umasikini, wakati chama tawala cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha Democratic kinaonekana kikipata nafasi ya tatu.
"Kumekuwa na msukumo kwa upande wa vuguvugu la 5-Star katika siku za mwisho za kampeni, lakini ni vigumu kuona chama chochote ama muungano wa vyama ukipata asilimia 40 zinazohitajika kuunda serikali," amesema Lorenzo Pregliasco, muasisi mwenza wa shirika la utafiti wa maoni ya wapiga kura la YouTrend.
Madeni ya taifa
Italia ambayo ina madeni mpaka shingoni ni uchumi wa tatu katika mataifa 19 ya kanda ya sarafu ya euro na licha ya kwamba wawekezaji wamekuwa wenye matumaini kabla ya uchaguzi wa leo, mkwamo wa kisiasa uliorefushwa unaweza kufufua kitisho cha kutokuwa na uthabiti wa masoko.
Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa kuanzia saa moja asubuhi leo hadi saa tano usiku , ambapo matokeo ya awali yanatarajiwa mara tu baada ya vituo kufungwa. Uchaguzi huo unafanyika chini ya sheria mpya ya uchaguzi yenye utata ambayo ina maana matokeo ya mwisho huenda hayatakuwa wazi hadi Jumatatu.
Kampeni zimeshuhudia kurejea katika mstari wa mbele wa siasa Berlusconi mwenye umri wa miaka 81, ambaye alilazimika kuachia wadhifa wa waziri mkuu mwaka 2011 wakati wa mzozo mkubwa wa madeni ya ndani na aliondolewa kutokana na mlolongo wa kashfa za ngono, mivutano ya kisheria pamoja na afya mbaya.
Hukumu ya mwaka 2013 kwa udanganyifu wa kulipa kodi ulikuwa na maana hawezi tena kuwa kiongozi wa umma na amemuweka mbele Antonio Tajani, Rais wa bunge la Ulaya , kuwa mgombea wa kiti cha waziri mkuu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Caro Robi