1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataliban wasonga mbele kijeshi huko Pakistan

Miraji Othman23 Aprili 2009

Wataliban waiteka wilaya nchini Pakistan

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Hilary Clinton.Picha: AP

Wapiganaji wa Kitaliban jana waliidhibiti wilaya ilioko kilomita 110 kutoka mji mkuu wa Pakistan, Islamabad, huku wakipiga doria mabarabarani na masokoni. Mamia ya wapiganaji hao waliweka vizuwizi majiani na kuitwaa misikiti katika wilaya ya Buner, kaskazini magharibi ya Islamabad, kukiweko wasiwasi kote duniani kutokana na hali hiyo. Marekani imesema hali hiyo ni kitisho kwa Pakistan inayomiliki silaha za kinyukliya.

Wapiganaji hao wa Kitaliban waliingia mji wa Buner wakitokea Bonde la Swat ambako rais wa Pakistan, Asif Ali Zardari, alitia saini makubaliano yanayoruhusu kuweko mahakama za sheria za Kiislamu katika eneo hilo. Hiyo ilikuwa katika juhudi za kuzuwia kuenea michafuko mikubwa katika wilaya hiyo. Afisa mmoja wa polisi katika eneo hilo alisema Wataliban wanapiga doria mabarabarani, na pia maafisa wa serekali walikuwa wanafanya mazungumzo na Wataliban kuumaliza uvamizi huo wa kijeshi. Kamanda wa Taliban alisema wao wataunda mahakama za sheria za Kiislamu katika wilaya ya Buner kama walivofanya katika Bonde la Swat, lakini hawatajiingiza katika shughuli za polisi. Uvamizi huo wa kijeshi wa Wataliban umesababisha kuweko hofu miongozi mwa wakaazi wa wilaya hiyo.


Itakumbukwa kwamba serekali kuu ya Pakistan ilishindwa kulidhibiti Bonde la Swat, eneo ambalo zamani watu wanaokimbia juu ya barafu walipenda sana kulitembelea na lilikuwa almasi katika biashara ya utalii ya Pakistan, baada ya kuweko kampeni ya utumiaji nguvu iliodumu miaka miwili kushikilia kuweko sheria za Kiislamu. Serekali kuu ilikubali kuweko mahakama za aina hiyo katika wilaya ya Malakand, wilaya inayokaliwa na watu milioni tatu hivi katika mkoa wa Kaskazini Magharibi ili kuziwia kuenea michafuko.

Wataliban wakiwa na silaha kaliPicha: Faridullah Khan


Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Hilary Clinton, jana alisema kusonga mbele kijeshi Wataliban ni kitisho kwa uhai wa Pakistan; na aliwahimiza Wapakistan duniani kote walipinge jambo hilo. Jana, mbele ya kamati ya baraza la wawakilishi la bunge la Marekani, inyoshughulikia masuala ya kigeni, aliilaumu serekali ya Pakistan kwamba iliwapigia magoti Wataliban kwa kukubali kuweko sheria za Kiislamu katika Bonde la Swat. Alisema kwa kufanya hivyo serekali ya Islamabad ilipoteza uaminifu na imekubali kubinywa na Wataliban na watu wengine wenye siasa kali. Hata hivyo, Bibi Clinton alihoji kwamba dola ya Pakistan sasa haiwezi kuwa na mfumo wa sheria unaofanya kazi:

"Nafikiri serekali ya Pakistan, kimisngi, inawacha nafasi kwa Wataliban na watu wenye siasa kali. Lakini angalia namna jambo hilo linavofanyika. Ukizungumza na watu huko Pakistan, hasa katika maeneo yasiokuwa na serekali na ambayo yanazidi kwa idadi, hawaamini kwamba serekali ina mfumo wa mahakama wenye kufanya kazi."



Wakaazi katika wilaya hiyo wanasema wataliban walikuwa wanawaomba watu mabarabarani wawaunge mkono katika juhudi zao za kurejesha sheria za Kiislamu, huku matangazo katika vikuza sauti vya misikitini yakisema harakati zisizokuwa za Kiislamu hazitastahamiliwa tena. Mabiramu yalitundikwa katika mji yakiwaambia wanawake wasiende masokoni na mahala pa hadharani, pia wanaume wasinyowe nywele. Polisi waonesha kwamba hawana nguvu za kuizuwia hali hiyo.


Serekali kuu huko Islamabad imesema inatuma vikosi sita vya wanajeshi hadi Bruner, na baadhi ya vikosi hiyo vimewasili jana kulinda majengo ya serekali na madaraja. Pia imeripotiwa kwamba wapiganaji wenye siasa kali walikishambulia kituo cha malori katika mkoa huo wa kaskazini magharibi ya Pakistan na kuyachoma moto malori 5 yaliokuwa yanabeba mafuta kupelekewa majeshi ya NATO katika Afghanistan.


Kusonga mbele Wataliban katika Pakistan kunatokea wakati ambapo Rais Barack Obama wa Marekani anapanga kufanya mazungumzo mwezi ujao na viongozi wa Afghanistan na Pakistan.


Mwandishi: Miraji Othman/AFP

Mhariri: Mohammed Abdulrahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW