1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAsia

Watu 5 wafa baada ya ndege 2 kugongana na kuwaka moto Tokyo

2 Januari 2024

Watu watano wamefariki dunia baada ya ndege kubwa ya abiria ya shirika la ndege la Japan Airlines kugongana na ndege ya walinzi wa pwani iliyokuwa ikileta msaada kwa manusura wa janga la tetemeko la ardhi nchini Japan.

Japan | Ndege ya shirika la ndege la Japan, JAL, ikiwaka moto baada ya kugongana na ndege ya walinzi wa pwani kwenye uwanja wa Hanela
Ndege ya shirika la ndege la Japan, JAL, ikiwaka moto baada ya kugongana na ndege ya walinzi wa pwani kwenye uwanja wa Hanela, Tokyo, Januari 02, 2024.Picha: Issei Kato/REUTERS

Ndege hiyo ya abiria chapa ya Airbus A350, mara moja ilianza kuteketea kwa moto, lakini watu wote 379 waliokuwamo ndani waliweza kuondoka bila majeraha ya kutishia maisha, Shirika la Ndege la Japan (JAL) lilitangaza Jumanne baada ya ajali hiyo.

Hata hivyo vifo vya watu watano kwenye ndege ya walinzi wa pwani, ambayo pia ilishika moto, vimefunika juhudi za kuleta msaada kwa walionusurika na kuokoa watu kutoka kwenye vifusi vya tetemeko la ardhi kwenye pwani ya magharibi ya Japan.

Sababu ya ajali hiyo iliyotokea wakati wa utaratibu wa kutua kwa ndege ya abiria katika uwanja wa ndege wa Haneda wa Tokyo, bado haijafahamika. Ni rubani pekee wa ndege ya Bombardier DHC8-300 ya walinzi wa pwani aliyefanikiwa kutoka akiwa hai, lakini alipata majeraha mabaya.

Soma pia: Japan: Idadi ya vifo yaongezeka baada ya tetemeko la ardhi

Ndege hiyo ya walinzi wa pwani yenye makao yake uwanja wa Haneda ilikuwa kwenye njia ya kurukia ndege ilipogongana na ndege ya JAL mwendo wa saa kumi na moja na dakika 50 za jioni, vyombo vya habari vya Japan viliripoti. Njia zote za kurukia ndege katika uwanja huo wa ndege zilifungwa, kulingana na Wizara ya Uchukuzi.

Ndege ya shirika la ndege la Japan, JAL, ikiwaka moto baada ya kugongana na ndege ya walinzi wa pwani kwenye uwanja wa Hanela, Tokyo, Januari 02, 2024.Picha: Kyodo News/AP

Vituo vya Televisheni vya Japan viligeuka kutoka kuonyesha picha za uharibifu kwenye pwani ya magharibi ambako watu 55 walikufa, na kuanza kuonyesha picha za moja kwa moja za ndege ya abiria ikiteketea kwa moto katika uwanja wa ndege wa Tokyo.

Mashuhuda waelezea walichokishuhudia

Picha za shirika la utangazaji TBS zilionyesha abiria wa ndege hiyo ya kibiashara wakiondoka kupitia kitelezo cha dharura huku wazima moto wakipambana na moto huo.

Kila kitu kilianza kutikisika na taa zikazimwa, kulingana na walioshuhudia. "Ilikuwa kama hadithi ya kutisha," abiria wa Swedem Anton Deibe alikiambia kituo cha redio cha Sweden, SVT, baada ya kuhamishwa. Kijana huyo umri wa miaka 17 alikuwa ameketi karibu na dada yake nyuma ya bawa linalowaka moto wakati hofu ilipozuka ndani ya ndege, alisema.

Mwanamume wa Kijapani mwenye umri wa miaka 33 aliliambia gazeti la Asahi Shimbun kwamba miali ya rangi ya chungwa ilikuwa ikitoka nje ya dirisha huku ndani kukijaa moshi.

Soma pia: Tsunami yaipiga Japan

Yeye, kama wengine wengi waliokuwemo kwenye ndege, alikuwa akirejea kutoka kwenye sherehe za mkesha wa Mwaka Mpya, na alikuwa na mke wake na binti yake wa miaka 2 kwa wakwe zake huko Hokkaido. Maneno ya "tafadhali tulieni. Tafadhali mssichukue mizigo yanu," lyalikuwa yakioneshwa kwenye ubao, alisema mwanaume huyo wa Kijapan.

Ndege ya shirika la ndege la Japan, JAL, ikiwaka moto baada ya kugongana na ndege ya walinzi wa pwani kwenye uwanja wa Hanela, Tokyo, Januari 02, 2024.Picha: Kyodo News/AP

Wakati wazima moto walizima moto mkubwa karibu na mmoja ya injini zilizoharibiwa, huku mikali ikitokea kwenye madirisha ya ndege, abiria waliondoka kwenye ndege kupitia kitelezo cha dharura. Miongoni mwa waliotoroka ni watoto wadogo wanane na watu 17 waliokuwa ndani ya ndege hiyo walipata majeraha.

Ajali hiyo inakuja baada ya takriban watu 55 kuuawa na 137 kujeruhiwa katika tetemeko kubwa la ukubwa wa 7.6 katika siku ya mwaka mpya.

Chanzo: DPA