1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watanzania waanza kufurahia usafiri wa treni ya SGR

20 Juni 2024

Nchini Tanzania usafiri wa treni ya kisasa inayotumia umeme (SGR) umeanza. Treni hiyo iliwabeba abiria kutoka Dar es salaam hadi Morogoro na kurejea tena jijini humo.

SGR Tanzania
SGR itaanzisha mkondo mwingine mpya wa safari hadi Dodoma mwezi Julai mwaka huuPicha: Tanzania State House

Ni safari iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu na hatimaye leo mambo yametimia baada kukamilika hatua zote pamoja na majaribio yaliyofanyika kati ya Dar es salaam hadi Morogoro na baadaye majaribio hayo kufika hadi Dodoma.

Safari ya leo ya kilometa 300 imepokelewa kwa hisia mseto na baadhi ya wale waliotumia usafiri huo wengi wao wanasema ni hatua ya kupigia mfano inayofungua mapinduzi mapya katika sekta ya usafiri wa reli.

Safari ilianza saa 12 alfajiri kuelekea Morogo na ilipofika majira ya saa mbili kasorobo ilikuwa tayari imefika kituo chake cha mwisho na baadaye kuanza kurejea tena Dar es salaam ikiwa na abiria waliokamilisha safari yao mnamo majira ya saa nne na nusu. Abiria wanasema wamesafiri kwa utulivu na furaha tele.

Ama hatua hiyo ya kuanza safari za kusafirisha abiria inamaanisha kwamba huenda pia shughuli nyingine zikiwamo zile za kibiashara na hata kuwahi matibabu sasa zitakuwa zimerahisishwa.

Katika hali ya kawaida usafiri wa mabasi ya abiria kutoka Dar es salaam hadi Morogoro unaweza kuchukua muda wa saa zisizopungua tatu. Ujio wa treni hiyo ni habari njema pia kwa wakazi wa maeneo ya Morogoro.

Baadhi ya abiria wanasema treni hiyo ambayo pia inalenga kuziunganisha nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Rwanda na Burundi ni hatua inayoharakisha na kurahisisha shughuli za kibiashara.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa shirika la reli nchini, Masanja Kadogosa gharaza za usafiri huo zimegawanyika kulingana na aina ya usafiri, umbali wa eneo pamoja na mahitaji mengine yanayoweza kupatikana. 

Anasema kwa behewa la kawaida kutoka Dar e salaam hadi Morogoro inagharimu kiasi cha shilingi 13,000 lakini kiwango hicho kinaongezeka kwa abiria wanaopendelea treni za haraka.

Safari za Dar es salaam hadi Dodoma zinatarajiwa kuzinduliwa rasmi mapema mwezi ujao, na baadaye kuendelea kupisha uendelezaji wa kipande kingine kitakachoenda katika mikoa ya jirani hadi kufika huko Mwanza na maeneo mengine.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW