1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watanzania wataka elimu iboreshwe- Utafiti

Hawa Bihoga17 Mei 2018

Taarifa ya utafiti uliofanywa na shirika la TWAWEZA imeeleza kuwa wananchi tisa kati ya kumi nchini Tanzania sawa na asilimia 87 wanahitaji kuboreshwa kwa elimu hata kama watahitajika kulipa fedha.

Tabora Girls School in Tansania
Picha: DW/Z. Mussa

Nchini Tanzania, katika utafiti wa shirika lisilo la kiserikali la linalojihusisha na masuala ya tafiti za kijamii na kisiasa Twaweza, unaonesha wananchi tisa kati ya kumi wanahitaji elimu iboreshwe nchini  humo hata kama watahitajika kulipia fedha.

Utafiti huo uitwa Elimu Bora Au Bora Elimu? Umewahoji watu zaidi ya elfu moja na mia saba kwa Tanzania bara pekee unaonesha kuwa mitazamo ya wananchi kuhusu elimu bure imebadilika kwa kiasi kikubwa kwa takriban miaka kumi iliopita

Taarifa ya utafiti huo imeeleza kuwa mwaka 2005 zaidi ya nusu ya wananchi walihitaji elimu bure hata kama kiwango cha elimu kitakuwa chini hatua ambayo wanafunzi wengi zaidi walijiandikisha, lakini mwaka 2017 wananchi tisa kati ya kumi sawa na asilimia 87 walihitaji kuboreshwa kwa elimu hata kama watahitajika kulipa fedha.

Mashaka kuhusu ubora wa elimu

Asilimia 87 ya waliohojiwa walichagua kuwe na mpango wa mafunzo kwa walimu Picha: ONE/Restless Development

Utafiti huo umeendelea kuonesha kwamba wananchi wengi wanamashaka na ubora wa elimu unaotolewa kwa shule za umma ikiwa serikali ina nia ya kupambana na ongezeko la idadi ya wanafunzi ambao walikuwa na kikwao katika upatikanaji wa elimu.

Aidan Eyakuz mkurugenzi mtendaji wa twaweza amesem kuwa wananchi walipoulizwa kuhusiana na mpango wa serikali kugawa sare za shule bure kwa wanafunzi au mpango wa mafunzo kwa walimu asilimia 87 walichagua mpango wa mafunzo kwa walimu hatua alioitaja inaongeza ushahidi zaidi ya utayari wa wananchi kuchangia elimu nchini kwa matokeo bora.

Utafiti huu unaungwa mkono na shirika la Haki elimu ambalo limejikita kutetea maslahi ya elimu nchini kwa hoja kuwa bajeti ya elimu nchini huenda ikawa ni chagizo la kudidimia elimu kutokana na mahitaji kuongezeka na fedha inayotengwa na inayofikishwa haiwiani na kiasi cha mahitaji yanayohitajika katika sekta ya elimu nchini.

Mitazamo ya wananchi kuhusu elimu bure imebadilika kwa kiasi kikubwa kwa takriban miaka kumi iliopitaPicha: UNICEF/GIACOMO PIROZZI

Matokeo mema katika mitihani na miundombinu ya shule ni vivutio kwa wazazi

Utafiti umeendelea kuonesha kuwa, asilimia 72 ya wazazi wenye watoto wao wanaosoma shule za msingi huzingatia matokeo mazuri ya mtihani wa kidato cha nne na walimu wenye ari huku sifa nyingine kwa kaya ikiwa ni miundombinu mizuri na sifa nzuri ya shule hata bila kuthibitisha. Hili linatajwa na wananchi wenyewe kuwa linatokana na utashi wa kisiasa ambapo watunga sera hawafikirii matokeo ya sasa bali ni maneno ya kuwaridhisha wananchi ili kulinda nafasi zao mamlakani.

Hata hivyo walimu wenyewe wamesema kuwa hadi sasa juhudi kubwa za serikali zimeendelea kusalia katika kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu, lakini changamoto ya motisha kwa walimu bado inarudisha nyuma ari ya walimu kufundisha darasani hivyo kusalia ofisini hadi muda wa kurejea nyumbani hatua ambayo inazalisha matabaka ya kielimu kati ya matajiri na masikini.

Mwandishi: Hawa Bihoga Dw Dar es salaam

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW