1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watawala wapya Guinea watafuta kujiimarisha madarakani

7 Septemba 2021

Maafisa wa kijeshi nchini Guinea wamekutana kujadili makabidhiano ya madaraka. Katika mji mkuu wa Conakry kumeripotiwa hali ya utulivu lakini wasiwasi unaendelea kuwepo kuhusu uwezekano wa kutokea machafuko.

Guinea | Mamady Doumbouya
Picha: CELLOU BINANI/AFP/ Getty Images

Baada ya kuirejesha nchi hiyo ya Afrika Magharibi chini ya utawala wa kijeshi kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja, utawala wa kijeshi ulikuwa tayari umevunja bunge la taifa na kusitisha katiba.

Siku ya Jumatatu, makamanda wa kimkoa walichukua nafasi za magavana wa Guinea katika hatua ya utawala huo kuimarisha udhibiti wake.

Soma pia: Ulimwengu walaani mapinduzi ya kijeshi Guinea

Kiongozi wa kijeshi Kanali Mamady Doumbouya alisema utawala mpya wa kijeshi hautalipiza kisasi dhidi ya madui wa kisiasa, lakini pia aliwaagiza maafisa aliowaita kutoka serikali iliyopinduliwa yaAlpha Conde kukabidhi hati zao za kusafiria mara moja, na kusema wakati wa kipindi cha mpito, hakutakuwa na ruhusa ya kusafiri nje ya mipaka ya Guinea kwa mafisa hao wa serikali ya zamani.

Waziri mkuu wa Guinea Ibrahim Kassory Fofana, waziri wa ulinzi Moahamed Diane na mafisa wengine wa serikali wakiwa wamekusanyika kukutana na kamanda wa kikosi maalumu Mamady Doumbouya, aliempindua rais Alpha Conde mjini Conakry, Guinea, Septemba 6, 2021.Picha: Souleymane Camara/REUTERS

Mshauri wa masuala ya kiuchumi wa rais wa Guinea Sylla Naby Moussa, amesema kwa ujumla nchi hiyo inashuhudia hali ya utulivu na amani, lakini mashaka yanaendelea, baada ya kile alichoendelea kukiita jaribio la mapinduzi, na kuongeza kuwa kila kitu kinaanza upya sasa.

"Kwa ujumla tunaweza kusema kuna amani Guinea kwa sababu katika maeneo mengi ikiwemo mji mkuu Conakry, tunaona watu wanatoka kufanya shughuli zao za kawaida. Lakini kwa sasa hakuna lililo na uhakika, hakuna kilicho bayana," alisema Moussa.

Soma pia: Rais Alpha Conde apuuza shutuma za kuwaandama wapinzani

"Ukilinganisha na hali ya mwaka jana, hakuna visa vya ukosefu wa usalama kwa ngazi ya serikali na miongoni mwa watu."

Hakuna muda wa kuachia rais Conde

Rais aliepinduliwa Alpha Conde.Picha: AFP

Mashirika ya kimataofa kama Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Magharibi ECOWAS, pamoja na baadhi ya serikali ikiwemo China zimelaani mapindizi nchini Guinea, na kutaka rais Conde aachiwe mara moja.

Lakini utawala wa kijeshi umekataa kutoa muda wa kumuachia Conde, ukisema kuwa rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 83 bado anapata huduma za afya na yuko karibu na madaktari wake.

Soma pia: Milio ya risasi yasikika karibu na Ikulu Conakry

Kupinduliwa kwa Conde siku ya Jumapili kulijiri baada ya rais huyo kuwania na kushinda muhula wa tatu wenye utata mwaka uliyopita, akihoji kwamba ukomo wa mihula haukumhusu yeye.

Katika tamko lake la kwanza tangu mapinduzi, chama kikongwe cha upinzani cha National Alliance for Change and Democracy kilisema mapinduzi hayo ya Jumapili yanabeba matumaini ya mwanzo mpya kwa taifa hilo. Lakini kiliwahimiza pia wanajeshi kuanzisha haraka utawala wa sheria.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW