1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watawala wapya wa Burkina Faso waituhumu Ufaransa

Daniel Gakuba
2 Oktoba 2022

Waandamanaji wenye hasira wameshambulia ubalozi wa Ufaransa katika mji mkuu wa Burkina Faso, baada wa wafuasi wa wanajeshi waliofanya mapinduzi mapya kuituhumu Ufaransa kumpa hifadhi rais wa mpito aliyeangushwa.

Burkina Faso | Militärputsch
Picha: Assane Ouedraogo/EPA-EFE

Waandamanaji wenye hasira wameshambulia ubalozi wa Ufaransa katika mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou jioni ya Jumamosi, baada wa wafuasi wa wanajeshi waliofanya mapinduzi mapya kuituhumu Ufaransa kumpa hifadhi rais wa mpito aliyeangushwa. Marekani nayo imesema inafuatilia kwa wasiwasi mkubwa yanayojiri Burkina Faso.

Soma zaidi: Milio ya risasi yasikika nje ya makazi ya rais Burkina Faso

Luteni Kanali Paul Henri Sandaogo Damiba ambaye aliongoza mapinduzi mengine ya kijeshi miezi tisa iliyopita alitimuliwa Ijumaa jioni, na Ufaransa imekanusha vikali madai kwamba inampa ulinzi ama katika ubalozi wake, au katika kambi ya kijeshi.

Picha za vidio zilizowekwa katika mitandao ya kijamii zimeonyesha kundi la watu wenye mienge inayowaka moto wakiwa katika eneo linalouzunguka ubalozi wa Ufaransa mjini Ouagadougou.

Wanajeshi waliofanya mapinduzi walikwenda studio za televisheni kumtangaza kiongozi wao, Kapteni Ibrahim Traore kuwa rias mpyaPicha: RADIO TELEVISION BURKINA FASO/REUTERS

Damiba hajulikani aliko hadi

Hadi Jumamosi jioni ilikuwa bado haijajulikana mahali alipo kiongozi huyo mwanajeshi aliyetimuliwa. Katika tangazo lake wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa imesema, ''Tunakanusha rasmi kuhusika kwa aina yoyote ya matukio nchini Burkina Faso. Paul Sandaogo Damiba kamwe hajapewa hifadhi katika kambi zilizo na wanajeshi wetu, wala ubalozi wetu.''

Soma zaidi: ECOWAS yaziondolea vikwazo Mali na Burkina Faso

Kupitia mtandao wa kijamii wa twitter, Paul Henri Sandaogo Damiba amewataka wanajeshi walionyakua madaraka ''kutumia fikra timamu.''

Msemaji wa serikali ya Ufaransa  Anne-Claire Legendre amesema wanalaani kwa nguvu zote ghasia zinazoelekezwa kwenye ubalozi wao, na kuongeza kuwa ''Kitengo cha dharura kimeundwa mjini Ouagadougou na watu wetu wako tayari kuhakikisha usalama wa raia wa Ufaransa, ambao ndio wenye kipaumbele.''

Luteni Kanali Paul-Henri Damiba hajulikani alipo baada ya utawala wake kuangushwaPicha: BURKINA FASO PRESIDENCY/REUTERS

Kapteni Ibrahim Traore, ambaye alitambulishwa kama kiongozi wa mapinduzi mapya alionekana katika televisheni ya taifa Ijumaa jioni, na katika mahojiano yake ya kwanza alisema yeye na watu wake hawana mpango wa kumdhuru Damiba.

''Kama tungetaka tungemkamata katika muda wa chini ya dakika tano, na pengine angeuawa katika mapigano, lakini hatutaki janga hilo,'' alisema Traore. Mwanajeshi huyo pia aliiambia Sauti ya Amerika kuwa ''Hatutaki kumdhuru rais, kwa sababu hatuna matatizo na yeye binafsi. Tunapigana kwa ajili ya Burkina Faso.''

Hali ya usalama ni tete katika mji mkuu

Barabara za mjini Ouagadougou zimeendelea kufungwa na helikopta ilikuwa ikizungukazunguka angani. Tathmini ya ndani ya Umoja wa Ulaya iliyoonekana na shirika la habari la AP ilisema kulikuwapo ''shughuli za kijeshi zisizo za kawaida'' katika mji huo mkuu.

Marekani imejiunga na nchi zilizopasa sauti kulaani mapinduzi haya ya kijeshi nchini Burkina Faso, ikiyalaani mapinduzi hayo na kusema yanayojiri yanaleta wasiwasi mkubwa.

Soma zaidi: UN: Mapigano ya Sahel yataongeza wakimbizi zaidi Ulaya

''Tunaona kuwa kwa mara ya pili katika muda wa miezi minane, maafisa wa jeshi wamesema kuwa wamevunja serikali na kulifuta bunge na katiba,'' imesema Wizara ya Mambo ya Nje mjini Washington katika tangazo lake.

Tayari Umoja wa Afrika, AU pamoja na jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS vimekosoa vikali hatua ya wanajeshi wa Burkina Faso kuiangusha serikali.

''ECOWAS inapinga unyakuaji huu wa madaraka uliotokea wakati maendeleo yakianza kupatikana,'' imesema jumuiya hiyo, ikimaanisha makubaliano yaliyofikiwa na Damiba hivi karibuni ya kuirejesha Burkina Faso katika utawala wa kikatiba.

-ape, afpe

 

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi