Watayarishaji wa CeBIT 2005 wameridhika hata mwaka huu
15 Machi 2005Leo hii ikiwa ni siku ya tano ya maonyesho ya kimataifa ya kompyuta na njia za mawasiliano ya CEBIT, mkurugenzi wa shirika lililoandaa maonyesho haya Bwana ERNST RAUE amesema, anaridhika na tathmini iliyofanywa katikati ya maonyesho haya. Amesema hali inatia moyo kwa ustawi wa uchumi hapa nchini na duniani kote kwa ujumla, kwa vile makampuni yameanza tena kuwekeza pesa nyingi zaidi kwenye teknolojia mpya.
Katika kipindi cha siku tatu za kwanza, zaidi ya wageni 200,000 – kama ilivyokuwa mwaka jana --- walifika kwenye maonyesho haya yanayoongoza kwa ukubwa duniani. Hadi kufikia mwishoni mwa maonyesho haya, kesho kutwa tarehe 15-Machi, zaidi ya watu nusu milioni watakuwa wamefika hapa Hannover kujionea teknolojia mpya kwenye fani ya kompyuta na njia za mawasiliano.
Tafauti kubwa na mwaka jana ni kuwa, mara hii idadi ya viongozi wa makampuni, hususani kutoka katika nchi za nje, imeongezeka na kufikia robo ya wageni wote. Watayarishaji wa maonyesho haya ya kimataifa wamefurahia pia ongezeko la idadi ya wageni kutoka nchi za nje kwa asilimia 5 na kufikia asilimia 33 ya wageni wote. Mwaka huu peke yake wanatarajiwa wageni 16,000 kutoka Asia peke yake --idadi hii inaonyesha ongezeko la asilimia 35.
Kwa upande mwingie, wahusika wamesema, idadi ya watu wanaotumia mtandao wa Internet kupata habari mpya za maonyesho ya kompuyta, imeongezeka kwa asilimia 25 kwa kulinganisha na mwaka jana. Mihadhara na mazungumzo ya wataalamu na waandishi wa habari yanaweza kufuatiliwa kwa kwa video kupitia mtandao wa Internet. Tovuti ya maonyesho haya ni www.CEBIT.de
Mwaka huu makampuni 6,300 kutoka nchi 65 duniani yamewakilishwa kwenye maonyesho haya. Zaidi ya nusu ya makampuni haya ni ya uwezo wa wastani na yanatoka nje ya Ujerumani.
Kama kawaida, maonyesho ya kimataifa ya kompyuta na njia za mawasiliano ya kisasa CEBIT hupewa uzito mkubwa na wanauchumi na wanasiasa nchini Ujerumani, kwa vile hutumiwa kama kioo na dira ya ustawi wa uchumi. Mwaka uliopita ulikuwa mzuri kwa sekta hii: Uzalishaji wa kompyuta za matumizi ya kawaida uliongezeka kwa asilimia 7. Lakini kizungumkuti hapa ni kuwa, vifaa vingi vya kompyuta vinatengenezwa kwa bei nafuu katika nchi za Asia, hususani Uchina, Taiwan na Honkong. Hata hivyo wanasiasa hapa nchini ambao hufika kwa wingi kwenye maonyesho haya, wana matumaini kuwa sekta hii itasaidia kuongeza nafasi za kazi.
[KW: Mwelekeo mpya hivi sasa ni watu kununua kompyuta za bei nafuu lakini zenye uwezo sawa na kompyuta za bei kubwa, na hapohapo kuzitumia kwa muda mrefu zaidi. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa kwa kushirikiaana na gazeti la Handelsblat, bei za kompuyta zimepungua kwa asilimia 2 hivi.]
Mada muhimu kwenye maonyesho ya mwaka huu ni matumizi ya teknolojia mpya ya simu za mkononi UMTS ambayo iliasisiwa kwenye maonyesho haya CEBIT mwaka jana. Kwa kutumia teknolojia hii mpya, simu za mkononi zinaweza kutumiwa kwa mambo mengi zaidi, ikiwa ni pamoja na kutuma picha, video, kusikiliza muziki na kuangalilia Televisheni.
Teknolojia nyingine iliyopamba moto kwenye maoyesho ya CEBIT mwaka huu, ni teknolojia ya kupiga simu kupitia kwenye mtandao wa Internet. Voice-Over-IP yaani utumaji wa sauti kwa kutumia teknolojia ya Internet.