1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchuano wa Poland na Mexico, Lewandowski akosa peneti

23 Novemba 2022

Katika michuano ya kombe la dunia Ufaransa iliingia uwanjani kupambana na Australia bila ya wachezaji wake nyota Karem Benzema, Pogba na Kante na awali katika michuano ya kundi D Tunisia na Denmark zilitoka nguvu sawa.

Mshambuliaji hatari wa Poland Robert Lewandowski
Mshambuliaji hatari wa Poland Robert LewandowskiPicha: HAMAD I MOHAMMED/REUTERS

Ngoma ilianza kwa mshtuko kwa wafaransa. Mshambuliaji wa Australia aliliona lango la Wafaransa mnamo dakika ya 9 tu baada ya mechi kuanza lakini wafaransa walituliza makini na kuchanganya mashambulio yaliyoleta mavuno.

Katika dakika ya 27 Adrien Rabiot aliwatuliza moyo mashabiki wa Ufaransa kwa kusawazisha bao. Kabla ya kumalizika nusu ya kwanza mshambuliaji Giroud aliipatia Ufaransa bao la pili. Ufaransa iliendelea kuudhibiti mpira katika nusu ya kwanza ingawa Australia iliendelea kuwa hatari.

Mshambuliaji wa Ufaransa, Kylian Mbape aliyeifungia timu yake goli la tatu mnamo dakika ya 68.Picha: Markus Gilliar/GES/picture alliance

Nusu ya pili ilileta neema zaidi kwa watetezi wa taji baada ya mshambuliaji Kylian Mbape kufunga goli la tatu mnamo dakika ya 68. Wafaransa waliwazamisha Australia kwa uhakika kwa bao la nne lililofungwa na Giroud. Na hivyo kuipa Ufaransa ushindi wa mabao manne huku Australia ikiambulia bao moja. 

Hapo awali katika kundi hilo,la D Denmark na Tunisia pia ziliingia uwanjani zikiwa na nguvu sawa. Ulikuwa mchezo wa kwanza ambapo timu hazikufungana. Matokeo hayo yaliuambukiza mchezo wa pili. Vijana wa Ulaya kutoka Poland walitoka bila bila na timu ya Mexico. Mshambuliaji hatari wa Poland Robert Lewandowski bado anapaswa kusubiri mechi nyingine ili kuweza kutikisa wavu kwenye mashindano ya kombe la dunia baada ya mkwaju wa peneti aliopiga kupanguliwa na golikipa mahiri wa Mexico Guillermo Ochoa. Na kwa hesabu zote mashindao hayo ya kombe la dunia nchini Qatar ndiyo yatakuwa ya mwisho kwa mshambuliaji huyo wa Poland. Subira itavuta heri kwa Lewandowski.

Mchezaji Salem Al Dawsari Msaudi aliyewazamisha Argentina kwa kuwafunga bao la piliPicha: Ricardo Mazalan/AP Photo/picture alliance

Kwenye mashindano hayo ya nchini Qatar timu ya Saudi Arabia imeandika historia. Timu hiyo imewashangaza mashabiki wa soka kwa kuwaumbua Argentina kwa mabao mawili kwa moja katika mchezo wa kwanza wa kundi C.

Miamba ya soka ya Amerika kusini ilianza kwa matumaini baada ya mchawi wa kandanda Lionel Messi kuweka kabumbu kimiani kwa mkwaju wa peneti kwenye lango la Saudi Arabia. Lakini hiyo ilikuwa ni furaha ya samli juani kwani iliyeyuka. Vipanga wa Saudi Arabia walisawazisha dakika kumi baada ya nusu ya pili kuanza. Saleh Al Shehri aliutikisa wavu wa Argentina na mnamo dakika ya 53 Salem Al Dawsari aliwazamisha Waargentina kwa kufunga bao la pili. Kilikuwa kipenga cha mwisho kwa Argentina kwa mchezo wa jana lakini siyo kwa mashindano yote. Magoli matatu ya Argentina yalikataliwa kwa sababu yalikuwa ya kuotea! Hata hivyo Argentina bado imo miongoni mwa timu zenye matumaini ya juu ya kulibeba kombe la dunia. Muda bado upo.

Timu ya Argentina Lionel Messi namba 10Picha: Matthias Hangst/Getty Images

Katika mechi za leo Jumatano, Morocco itapambana na Croatia. Mabingwa wa dunia mara nne Ujerumani inakutana uwanjani na Japan. Nayo Uhispania itapimana nguvu na Costa Rica huku Ubelgiji ikiwa na miadi na Canada.

Chanzo:RTRE