1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto 13 katika nyumba ya mateso Marekani

16 Januari 2018

Binti mmoja wa miaka 17 amefanikiwa kujiokoa kutoka kwenye nyumba ambapo wazazi walikuwa wamemfungia yeye na dada na kaka zake 12. Watoto hao waliishi kwenye mazingira machafu, na baadhi walikuwa na utapiamlo.

USA Polizei mit Absperrband in San Diego
Picha: picture-alliance/dpa/.- Duenzl

Msichana huyo ambaye alikuwa na umbo dogo na maafisa polisi kuhisi alikuwa na miaka 10, alipiga namba ya dharura ya 911 na kupokelewa na polisi ambao walimuhoji na baadae kwenda kwenye nyumba hiyo, eneo la Perris, maili 70 kusini mashariki mwa Los Angeles.  

Mkuu wa idara ya polisi kwenye kaunti ya Riverside amesema walipofika kwenye nyumba hiyo walikuta baadhi ya watoto wakiwa wamefungwa na minyororo na kufuli kwenye vitanda vyao katika chumba kilicho na giza na harufu mbaya.

Baba wa watoto Allen Turpin Picha: Reuters/Riverside County Sheriff's Department

Watoto hao wa kati ya miaka 2 hadi 29 "walionekana kuwa na utapiamlo mkali na wachafu sana", hii ikiwa ni kulingana na taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari siku ya Jumapili iliyoelezea kukamatwa kwa wazazi wa watoto hao. "Watoto hao walipatiwa chakula na vinywaji baada ya kusema walikuwa na njaa."

Wazazi wa watoto hao David Allen Turpin, 57, na Louise Anna Turpin, 49, walikamatwa na kila mmoja kutakiwa kutoa dhamana ya Dola milioni 9, na wanaweza kukabiliwa na mashitaka ambayo ni pamoja na mateso na kuwaweka watoto katika mazingira ya hatari.

Mama wa watoto Louise Ann Turpin Picha: Reuters/Riverside County Sheriff's Department

Rekodi kutoka wizara ya mambo ya ndani ilionyesha nyumba hiyo ya familia ilikuwa na anuani inayofanana na shule ya kutwa ya Sandcastle, ambayo David Turpin anaonekana kuwa ni mkuu wa shule. Katika muhula wa masomo wa mwaka 2016-17, iliwaandikisha wanafunzi sita, katika madaraja sita ya shule hiyo, hivyo kila daraja likiwa na mwanafunzi mmoja.

Mwandishi: Lilian Mtono

Mhariri: Elizabeth Shoo