1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto 85,000 huenda walikufa Yemen kwa njaa na magonjwa

Sylvia Mwehozi
21 Novemba 2018

Shirika la msaada la Save the Children, limesema kiasi ya watoto 85,000 walio na umri chini ya miaka 5 huenda walikufa kutokana na njaa na magonjwa tangu kuanza kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen mwaka 2015.

Yemen - Kinder bei Camp in Sanaa
Picha: picture-alliance/Photoshot/M. Mohammed

Takwimu hizo ni kulingana na viwango vya vifo vya kesi ambazo haziku shughulikiwa za ugonjwa wa utapiamlo miongoni mwa watoto wadogo. Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watoto milioni 1.3 wamekabiliwa na utapiamlo tangu muungano unaongozwa na Saudi Arabia uingie katika vita ya Yemen dhidi ya waasi wa Kihouthi.

Save the Children inakadiria kwamba watoto 84,701 huenda walikufa kulingana na utafiti uliobaini kwamba kati ya asilimia 20 na 30 ya kesi ambazo haziku shughulikiwa zilisababisha vifo. Linasema mahesabu hayo yanatokana na kesi zilizoripotiwa kwenye maeneo ambako makundi ya misaada yalishindwa kuingilia kati.

"Kila mtoto anayeuawa na bomu na risasi, wengine kadhaa wanakufa kwa njaa kali na ni suala linalozuilika", alisema Tamer Kirolo, ambaye ni mkurugenzi wa shirika hilo nchini Yemen.

Vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vimegeuka moja ya mgogoro mbaya wa kiutu duniani. Robo tatu ya wakazi wa Yemen wanahitaji usaidizi wa kuokoa maisha na zaidi ya milioni 8 wako katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa. Maelfu ya watu wanaaminika kuuawa katika vita hiyo.

Save the Children inasema kuenea kwa baa la njaa, kumechangiwa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia kuzuia njia ya raia kutoka,  mwaka mmoja uliopita baada ya waasi wanaofungamna na Iran kurusha kombora kwenye mji mkuu wa Saudi wa Riyadh.

Mama akijitahidi kumlisha mtoto wake anayekabiliwa na utapiamloPicha: DW/J. Abdullah

Shirika hilo pia limebainisha mapigano ya karibuni ndani na nje ya mji wa bandari wa Hodeida, eneo ambalo ndiyo njia kuu ya kuingizia karibu asilimia 70 ya chakula na misaada ya kiutu.

Linasema uagizaji wa bidhaa kupitia bandari hiyo inayoshikiliwa na waasi umeshuka kwa mwezi kiasi cha kushindwa kukidhi mahitaji ya watu milioni 4.4. Kutokana na hilo, save the children sasa inalazimika kuingiza bidhaaa kwa ajili ya Yemen kaskazini kupitia bandari ya Kusini ya Aden, na hivyo kuchelewesha usambazaji.

Athari za mauaji ya mwandishi wa habari wa Saudia Jamal Khashoggi katika ubalozi wa nchi hiyo mjini Istanbul, zimemulika upya vita na kuleta taharuki nchini Yemen. Marekani imepunguza uungaji wake mkono muungano huo na kutaka usitishaji mapigano ifakapo mwisho wa mwezi huu.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Martin Graffiths anesema pande zote zimekubali kuhudhuria mazungumzo ya amani hivi karibuni na tayari ametembelea mji mkuu wa Sanaa ulio mikononi mwa waasi kwa ajili ya mazungumzo na kiongozi wa waasi wa Kihouthi siku ya Jumatano.

Lakini mapigano yanazidi kupamba moto mjini Hodeida na maeneo mengine na jitihada za mazungumzo ya amani zilizopita zimeshindwa kufikia makubaliano ya kusimamisha vurugu.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW