1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto katika ukanda wa Afrika Magharibi wako hatarini

27 Mei 2020

Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yameonya kuwa kizazi cha watoto wa Afrika Magharibi kinakabiliwa na hatari ya kukosa elimu muhimu na huduma za afya kutokana mizozo inayoendelea katika mataifa ya kanda hiyo.

Afrika Goma Kongo Kindersoldaten Resozialisierung
Picha: © UNICEF/NYHQ2011-0351/Asselin

Mustakabali wa idadi kubwa ya watoto katika eneo la Afrika Magharibi uko gizani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Amnesty International, watoto wengi wanaoishi katika maeneo kunakoshuhudiwa mizozo wako hatarini kukosa elimu na huduma za kimsingi kama vile afya.

Ripoti hiyo imeilaumu mamlaka nchini Nigeria kwa kukosa kuwalinda na kutoa elimu kwa watoto wanaoishi mashariki mwa nchi hiyo, sehemu ambayo imeathirika vibaya kutokana na vita vya zaidi ya muongo mmoja kati ya kundi la wapiganaji la Boko Haram na serikali ya Nigeria.

Ripoti ya Amnesty International iliyopewa jina "Tumekausha machozi Yetu" inalituhumu jeshi la Nigeria kwa kuwazuilia kinyume cha sheria watoto ambao walitoroka mikononi mwa Boko Haram.

Kaimu mkurugenzi anayeshughulikia mizozo katika shirika hilo Joanne Mariner, amesema:

"Mzozo baina ya jeshi la Nigeria na Boko Haram umeathiri zaidi watoto. Pia inaskitisha jinsi jeshi linavyowashugulikia kwa ukatili watoto waliotoroka mikononi mwa Boko Haram"

Hata hivyo, jeshi la Nigeria limekanusha tuhuma hizo.

Mwanaharakati wa kutetea haki za watoto nchini Nigeria Zariyatu Abubakar ameiambia DW kuwa watoto waliotoroka kutoka Boko Haram wanapaswa kupewa ulinzi na msaada wa serikali.  

Mashambulizi ya makundi ya wapiganaji yanatajwa kuathiri pakubwa elimu ya watoto

Watoto wakipokea mafunzo katika shule ya muda mjini Socoura, MaliPicha: picture-alliance/AP Photo/UNICEF/Dicko

Wakati huo huo, ripoti nyingine iliyotolewa na Human Rights Watch imeonyesha kumekuwa na ongezeko la mashambulizi yanayofanywa na makundi ya wapiganaji wenye itikadi kali nchini Burkina Faso tangu mwaka 2017. Mashambulizi hayo yanatajwa kuathiri pakubwa elimu ya watoto nchini humo.

Makundi ya silaha na yenye mafungamano na mitandao ya kigaidi ya Al-Qaeda na kundi linalojiita dola ya Kiislamu IS yamekuwa yakishambulia waalimu na shule, wakitoa sababu za kupinga mfumo wa elimu ya magharibi.

Human Rights Watch inasema pia mizozo na ghasia zimekithiri nchini Mali na Niger na kulazimisha shule kufungwa. Hali hiyo imewaacha watoto katika hatari kubwa ya kusajiliwa kama wapiganaji katika makundi ya kigaidi.

Shirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikia watoto Unicef, limesema kuwa karibu watoto milioni 8 wamelazimika kuacha shule kutokana na kuongezeka mashambulizi katika ukanda wa Sahel.

Takriban shule 3,000 zililazimika kufungwa katika eneo hilo kati ya Aprili 2017 na Disemba 2010. Shule 1,261 zilifungwa nchini Mali ilhali shule 354 zilifungwa nchini Niger.

Unicef inasema kuwa ukanda wa Sahel umekuwa kama kiini cha ghasia na mashambulizi yasiokuwa na kikomo.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW