1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto kumi waokolewa kutoka pangoni Thailand

Sylvia Mwehozi
10 Julai 2018

Wapiga mbizi huko Thailand wameanza awamu ya tatu ya kuwaokoa wavulana waliosalia kwenye pango lililofurika mafuriko walimokuwa wamekwama zaidi ya wiki mbili huko kaskazini mwa nchi hiyo.

Bildergalerie Thailand Höhlenrettung
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Lalit

Hadi kufikia sasa jumla ya wavulana 10 wameokolewa.Kwa mujibu wa maafisa wa afya, wavulana wanane waliookolewa ndani ya siku mbili zilizopita wanasemekana kuwa katika 'ari kubwa' na wana kinga imara kwasababu ni wachezaji wa mpira. Madaktari wamekuwa na tahadhari kwasababu ya hatari ya kupata maambukizi na wamewatenga watoto hao hospitali.

Waokoaji wakiwa ndani ya pango huko ThailandPicha: picture-alliance/AP Photo/Tham Luang Rescue Operation Center

Gavana wa Chiang Rai, Narongsak Osatanakorn amesema kwamba Operesheni ya kuwaokoa siku ya Jumanne imeanza saa 10 alfajiri na inahusisha wapiga mbizi 19. Timu ya madaktari na wanajeshi wanamaji watatu wa Thailand ambao walikaa na wavulana hao katika eneo dogo kavu ndani ya pango nao watatoka.

"Tunatarajia kama hakuna kitakachozuia, nathibitisha kwamba watoto wanne, kocha mmoja , madaktari na maafisa watatu wanamaji ambao walikuwa na watoto tangu siku ya kwanza walipowapata, watatoka nje ya pango leo. "

Gavana huyo amesema operesheni ya leo inaweza kuchukua muda mrefu tofauti na zilizopita ambazo zilitumia masaa 11. Hali ya wavulana hao na kocha wao imevuta hisia za wananchi wa Thailand na duniani kote, kutoka taarifa ya kupotea kwao hadi kutolewa kwa mkanda wa vidio wa kwanza ulionyesha kuwa wamepatikana na wako hai siku 10 baadae na wapiga mbizi wa kutoka Uingereza.

Walikwama katika pango la Tham Luan Nang Non ambalo lilifurika mafuriko kutokana na mvua za masika wakati walipokuwa wakifanya mazoezi ya mpira Juni 23.

Katibu mkuu wa wizara ya afya Thailand Jesada Chokedamrongsuk Picha: Getty Images/AFP/L. Suwanrumpha

Katika mkutano na waandishi wa habari, katibu mkuu wa wizara ya afya, Jesada Chokdumrongsuk amesema wavulana wanne wa kwanza waliokolewa walikuwa na umri wa kati ya miaka 12 na 16 na tayari wameanza kula kikawaida. Wawili kati yao wana uwezekano wamepata maambukizi katika mapafu lakini kwa ujumla wavulana wote nane wako katika "afya njema na wanatabasamu". "Kundi la pili lililotolewa jana ni umri kati ya miaka 12 na 14. Mmoja ana kiwango cha chini cha mapigo ya moyo na joto la chini la mwili. Tuliwapa dawa na sasa wao wanarejea katika hali ya kawaida. Asubuhi hii waliweza kuwasiliana vizuri, hawana homa na tumeanza kuwapa chakula maalum cha matibabu, " alisema Jesada.

Familia na ndugu wameweza kuwaona vijana hao angalau kutokea mbali kwasababu madkatari wanachukua tahadhari zote. Jesada anasema bado haijawa wazi wavulana hao wamepata maambukizi ya aina gani, "kwasababu hawajawahi kupitia hali kama hii ndani ya pango refu".

Gari ya kubebea wagonjwa imeshuhudiwa ikiondoka leo katika eneo la pango ambako shughuli ya uokoaji inaendelea na taarifa za punde ni kwamba mvulana mmoja tayari ametolewa. Kiasi ya magari tisa ya kubebea wagonjwa yalikuwa yakisubiri nje ya pango hilo. Na madaktari wamesema vijana hao huenda wakashindwa kuhudhuria mwaliko maalumu waliopewa wa kushuhudia fainali za kombe la dunia mjini Moscow.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP/AFP

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW